
Viongozi wa upinzani nchini DRC, Martin Fayulu, Delly Sesanga, Jean-Marc Kabund, na Ados Ndombasi wamejeruhiwa siku ya Alhamisi, Juni 12, huko Kinshasa wakati wa maandamano yaliyoandaliwa na muungano wa upinzani “C64” dhidi ya marekebisho ya katiba ambayo yatamwezesha Félix Tshisekedi kuhudumu muhula wa tatu.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Waandaaji, waliotoa taarifa hii, pia waliripoti majeraha kadhaa miongoni mwa waandamanaji. Pia walitaja vifo. Hata hivyo, idadi hii ya vifo haikuweza kuthibitishwa na vyanzo huru au mamlaka ya jiji .
Maandamano hayo, yaliyopangwa kama mkusanyikowa mati wa watu mbele ya makao makuu ya Bunge, yalipigwa marufuku siku iliyopita na mamlaka ya jiji la Kinshasa.
Kulingana na Prince Epenge, msemaji wa muungano wa “C64”, wafuasi zaidi ya 20,000 walihamasishwa kushiriki katika maandamano hayo. Anadai kwamba vyombo vya sheria viliingilia kati kuwatawanya waandamanaji.
Ili kudhibiti umati, polisi walitumia gesi ya kutoa machozi na kufyatua risasi kadhaa kuwaonya waandamanaji, na kusababisha hofu na usumbufu mkubwa wa shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na usafiri katika eneo hilo.
Asubuhi hali ilikuwa tulivu kabla ya mvutano
Asubuhi hali ilikuwa tulivu, licha ya uwepo mkubwa wa vikosi vya usalama vilivyopiga kambi pembezoni mwa makao makuu ya Bunge. Maafisa Polisi wa DRC walitumwa kwenye barabara kuu zinazoelekea makao makuu ya Bunge kuzuia mikusanyiko yoyote.
Hali ilizidi kuwa mbaya alasiri mapema wakati wanaharakati wa upinzani, waliokusanyika katika makao makuu ya chama cha upinzani cha ECiDé kwenye barabara kuu, Boulevard Triomphal, walijaribu kuandamana kuelekea makao makuu ya Bunge.
Baada ya zaidi ya saa moja ya mzozo na vikosi vya usalama, waandamanaji hatimaye walisukumwa kurudi nyuma mita mia kadhaa kutoka Bungeni.
Serikali bado haijasema chochote kuhusiana na matukio haya.