Dar es Salaam. Msanii maarufu wa muziki nchini Uganda, Joseph Mayanja ‘Jose Chameleone’, ametakiwa kulipa Sh7.5 milioni za Uganda sawa na Sh5 milioni za Tanzania kila mwezi. Kwaajili ya matunzo ya watoto wake watano, kufuatia makubaliano ya talaka kati yake na aliyekuwa mke wake, Daniella Atim.

Makubaliano hayo yalifikiwa Mei 2026 kupitia mchakato wa usuluhishi ulioidhinishwa na Mahakama Kuu ya Uganda chini ya jaji Jane Okuo Kajuga wa Kitengo cha Familia.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo. Daniella ataendelea kuwa mlezi mkuu wa watoto wao watano ambao ni Abba, Alpha, Amma, Alba na Xara. Huku Chameleone akipewa haki ya kuwaona watoto hao kwa kuzingatia utaratibu uliokubaliwa na pande zote mbili.

Chameleone na Daniella walifunga ndoa Juni, 2008. Lakini maisha yao ya ndoa yaligubikwa na migogoro ya muda mrefu iliyosababisha Daniella kuhamia Marekani pamoja na watoto wao zaidi ya miaka mitano iliyopita.

Katika madai yake ya talaka, Daniella alidai kuwa ndoa yao ilivunjika kutokana na kutengwa, ukatili wa ndoa na usaliti. Mambo aliyoyataja kuwa chanzo kikuu cha kuvunjika kwa ndoa hiyo baada ya zaidi ya miaka 17 ya kuwa pamoja.

Jose Chameleone ni mmoja wa wasanii wakubwa na wenye ushawishi mkubwa katika muziki wa Afrika Mashariki. Akiwa ametamba na nyimbo mbalimbali zilizovuka mipaka ya Uganda na kupata umaarufu mkubwa nchini Tanzania na kwingineko barani Afrika. 

Miongoni mwa nyimbo zake maarufu ni Valu Valu, Wale Wale, Mateeka, Jamila na Tubonge. Katika safari yake ya muziki, Chameleone amewahi kushirikiana na wasanii kadhaa wa Tanzania akiwemo marehemu nguli wa Bongo Fleva, Albert Mangwea,  Professor Jay, AY na wasanii wengine.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *