Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 6
Maandamano nchini India yalianza na wasiwasi miongoni mwa mamilioni ya vijana baada ya kughadhabishwa na uvujaji wa mitihani.
Wengi wao wakihofia maisha yao ya mbeleni iwapo mitihani inayoweza kuamua mustakabali wa Maisha yao haiaminiki tena basi wataiweka Imani yao wapi?
Kuanzia tarehe 20 mwezi Julai, makumi ya maelfu ya vijana wa kiume na wa kike waliandamana kuelekea katika jengo la Bunge la India. Polisi waliwatawanisha kwa kutumia mabomu ya machozi na marungu. Ila siku zinavyosonga, maelfu ya watu Zaidi wamejiunga na maandamano hayo.
Cockroach Janta Party (CJP), vuguvugu linaloongozwa na vijana lililoibuka kutokana na hasira kuhusu mfululizo wa uvujaji wa mitihani, limekuwa kwa kasi sana na kuchochea wimbi kubwa la uhamasishaji wa wanafunzi nchini India.
Vuguvugu hilo linataka mageuzi katika mfumo wa elimu na linataka Waziri wa Elimu, Dharmendra Pradhan, ajiuzulu.
Kiongozi mkuu wa vuguvugu hilo ni mwanaharakati Sonam Wangchuk, ambaye anasema alipoteza kilo 11 baada ya kufanya mgomo wa kula wa siku 26 kuunga mkono vuguvugu hilo.
Alimaliza mgomo wake wa kula jioni ya Julai 23, lakini viongozi wa wanafunzi walisema maandamano yataendelea hadi madai yao yatakapotekelezwa.
Swali ni Je, haya yalikuwa maandamano ya wanafunzi tu, au ni mwanzo wa jambo kubwa zaidi?
Vuguvugu la wanafunzi limewahi kubadilisha mara kadhaa mwelekeo wa kisiasa nchini India. Vuguvugu la Nav Nirman katika jimbo la Gujarat lilisaidia kuchochea kampeni iliyoanzishwa miaka ya 1970 na mwanasiasa mkongwe wa kisosholisti Jayaprakash Narayan, dhidi ya Waziri Mkuu wa wakati huo Indira Gandhi.
Hata hivyo, pia kumekuwa na vuguvugu nyingi ambazo zilizuka kwa nguvu kubwa lakini zikafifia haraka.
Chanzo cha picha, Reuters
Kinachoitofautisha CJP si ukubwa wake pekee, bali pia aina na upeo wa malalamiko yanayowakilishwa na vuguvugu hilo.
Tofauti na maandamano mengine makubwa yaliyofanyika dhidi ya serikali ya Waziri Mkuu Narendra Modi katika muongo uliopita iwe kuhusu sheria za uraia, sheria za kilimo au sera nyingine zenye utata vuguvugu hili halichochewi kimsingi na tofauti za kiitikadi. Wala haliwakilishi maslahi ya jamii au kundi fulani la kijamii.
Badala yake, vuguvugu hili linahoji iwapo serikali bado inaweza kuhakikisha usawa na haki katika mfumo wa mitihani mfumo ambao mamilioni ya vijana wa India wanaona kuwa ndiyo fursa yao muhimu zaidi ya kubadili hadhi yao ya kijamii na kiuchumi.
“Mfumo wa elimu na mitihani, kwa kiasi kikubwa, unavuka mipaka ya tabaka, hadhi ya kijamii na jinsia,” Yamini Aiyar, mtafiti mwandamizi mgeni katika Chuo Kikuu cha Brown, aliiambia BBC. “Wanaoshiriki maandamano haya hawawakilishi kundi moja maalum lenye maslahi yanayofanana.”
Utofauti huo pia ndio unaoipa vuguvugu hili sura yake ya kipekee kisiasa.
Rahul Verma, mtafiti katika Centre for Policy Research iliyoko Delhi, aliiambia BBC kuwa ” serikali kushindwa kuendesha mitihani kwa haki na kuzuia kuvuja kwa mitihani kunafanya hili kuwa changamoto tofauti kabisa ya kisiasa kwa chama tawala cha BJP.”
Mtafiti huyo anaeleza kuwa tofauti hii imebadili mazingira ya kisiasa. Tofauti na maandamano ya awali, ambayo mara nyingi yalitokana na tofauti za kiitikadi au kutokubaliana na sera fulani, vuguvugu hili linahoji uwezo wa BJP kuongoza na kusimamia serikali.
“Watalazimika kubadili mkakati wao,” Verma alisema.
Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, wengi wa wanaoshiriki maandamano haya hawakuwa wapinzani wa BJP hapo awali.
Ni “vijana wenye matarajio ya kupiga hatua kimaisha, na wazazi wao wanaona mitihani hii kama njia ya kujiendeleza.”
Kwa kuwa suala hili linatokana na utendaji wa serikali badala ya itikadi, huenda chama tawala cha BJP itapata ugumu kuhamasisha uungwaji mkono au kutumia jumbe zenye mgawanyiko wa kisiasa kama ilivyofanya katika maandamano ya awali.
Chanzo cha picha, Reuters
Katika kipindi cha wiki mbili zilizopita, watu wengi wameilinganisha CJP na vuguvugu la kupinga ufisadi la mwaka 2011, hasa kutokana na uwezo wake mkubwa wa kuwafikia watu kupitia mitandao ya kijamii. Hata hivyo, wakosoaji wamekuwa wakihoji iwapo msukumo huo wa kidijitali unaweza kuhamia kutoka mtandaoni na kuwatoa watu kwa wingi mitaani. Ukubwa wa maandamano ya Julai 20 unaonyesha kwamba hilo linawezekana kabisa.
Joyojit Pal, profesa katika Chuo Kikuu cha Michigan anayebobea katika teknolojia na jamii, anasema mitandao ya kijamii kwa sasa ni kama “pipa la baruti linalosubiri cheche ili kulipuka,” ambapo kasi ya kusambaa kwa taarifa na kiwango cha ushawishi wake huchochewa na hisia za watu.
Swali sasa ni iwapo wimbi hili la mtandaoni limegeuka kuwa vuguvugu la kudumu na lenye nguvu.
“Ninaamini maandamano ya Julai 20 yanaonyesha kwamba vuguvugu hili huenda limefikia hatua muhimu ya mabadiliko,” mtafiti Verma alisema.
Kwa maoni yake, iwapo vuguvugu hilo litaendelea kukua kutategemea kwa kiasi kikubwa namna serikali ya India itakavyojibu.
Chanzo cha picha, Hindustan Times via Getty Images
Baada ya kuwaachia mawaziri na wasemaji wa chama kujibu suala hilo, uongozi wa juu wa chama tawala cha BJP uliingilia moja kwa moja tarehe 22 Julai.
Waziri wa Ulinzi Rajnath Singh alikishutumu chama cha upinzani kwa kuwatumia wanafunzi “kama chombo cha kisiasa,” huku akisisitiza kuwa serikali imejitolea kushughulikia malalamiko yao kupitia bunge.
Waziri Mkuu Narendra Modi alizungumzia suala hilo hadharani kwa mara ya kwanza tarehe 23 mwezi Julai.
“Hakuna jambo muhimu zaidi kuliko ustawi na mustakabali wa kizazi cha vijana,” kiongozi huyo wa India aliandika kwenye mtandao wa kijamii wa X, huku pia akitangaza kuanzishwa kwa mahakama za kushughulikia kesi kwa haraka ili kuhakikisha “adhabu kali na ya haraka” kwa waliohusika na uvujaji wa mitihani.
“Wale wanaopanga njama za kuharibu mustakabali wa kizazi cha vijana wetu watachukuliwa hatua,”
Hata hivyo, bado haijulikani iwapo ahadi hizo zitatosha kukomesha wimbi la maandamano.
Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Mwanasayansi wa siasa Suhas Palshikar anasema huenda Vuguvugu la Cockroach likawa tu jukwaa la watu kutoa hasira zao kabla hali kutulia taratibu, kama ilivyotokea katika baadhi ya vuguvugu za awali za wakulima.
“Vuguvugu la Cockroach litaelekea wapi? Pengine hakuna popote litaruhusu watu kutoa hasira na kukatishwa tamaa kwao, kisha litafifia,” aliandika kwenye X.
Pia alionya dhidi ya kulipa vuguvugu hilo taswira ya kimapenzi kama uasi wa kizazi cha Gen Z.
Aliongezea kuwa “mwelekeo wa kiitikadi na kisiasa… [wa vuguvugu hilo] kwa sasa unabadilika,” na kwamba makundi mbalimbali ya kisiasa huenda yakajaribu kupata ushawishi ndani yake.
Hata hivyo, alisema jambo moja ambalo waandamanaji wamelionyesha wazi ni utayari wao wa kukabiliana na serikali.
“Vijana wameonyesha hasira na kutoridhika kwao. Wamekumbwa na ukandamizaji mkali wa polisi chini ya serikali ya kidemokrasia. Pia wameonyesha kwamba ni kwa kujitokeza mitaani pekee ndipo wanaweza kuilazimisha serikali hii… kuwasikiliza na kushiriki katika mazungumzo.”
Kwa mujibu wa Palshikar, iwapo nguvu hiyo ya vijana itaweza kudumu itategemea mambo mengi, yakiwemo ukandamizaji wa serikali, vikwazo vya upatikanaji wa taarifa kwenye vyombo vya habari, changamoto za uongozi wa vuguvugu hilo na ugumu wa kujenga muungano mpana wa kijamii.
Mwanauchumi Surajit Mazumdar wa Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru mjini Delhi pia anaamini kwamba vuguvugu hilo linaakisi jambo kubwa zaidi kuliko suala la kuvuja kwa mitihani.
Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
“Maandamano ya sasa na mwitikio wa hiari ambao yanaonyesha kutoridhika ulikokithiri miongoni mwa vijana na wanafunzi kuhusu hali ya nchi na mfumo wa elimu, jambo ambalo linakwenda mbali zaidi ya suala la kuvuja kwa mitihani,” aliiambia BBC.
Ikilinganishwa na vuguvugu za wanafunzi zilizotangulia, anaamini wimbi la sasa “ni pana zaidi na lina ukubwa mkubwa zaidi.”
Bw. Mazumdar pia alipinga dhana kwamba maandamano haya yamevuka mipaka ya itikadi. Kama ilivyokuwa kwa vuguvugu za awali za wakulima, alisema, maandamano haya yanaonyesha kwamba “roho ya demokrasia bado iko hai katika jamii ya India.”
Kwa Aiyar, msukumo huo wa kidemokrasia umeendelea na unaendelea kubadili sura ya siasa nchini India.
Iwapo hili litakuwa urithi mkubwa zaidi wa maandamano yaliyoanzishwa na Cockroach People’s Party, au litabaki kuwa maandamno ya muda mfupi wa hasira za umma, bado haijulikani.