Dodoma. Serikali imesajili wafanyabiashara ndogondogo 143,053 tangu kuanza kwa hatua hiyo Machi 2024, huku 8,426 wakinufaika na mikopo yenye masharti nafuu yenye thamani ya Sh17.9 bilioni.

Takwimu hizo zimetolewa leo Juni 1, 2026 bungeni na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk Doroth Gwajima wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/27.

Dk Gwajima amesema katika kipindi cha Julai 2025 hadi Aprili 2026, wafanyabiashara ndogondogo 56,039 walisajiliwa, wakiwemo wanaume 25,589 na wanawake 30,450.

Amesema hadi sasa idadi ya wafanyabiashara waliosajiliwa imefikia 143,053, ambapo wanaume ni 57,221 na wanawake 85,832.

Kwa mujibu wa waziri huyo, wafanyabiashara 63,246 wamelipia gharama za uchapishaji wa vitambulisho vya kidijitali na kati yao 51,333 sawa na asilimia 81.2 tayari wamekabidhiwa vitambulisho hivyo.

Amesema vitambulisho vya kidijitali vinabeba taarifa muhimu za biashara, eneo la biashara na shughuli za kiuchumi za muhusika, tofauti na kitambulisho cha Taifa ambacho kina taarifa binafsi za mwananchi.

Dk Gwajima amesema mfumo huo umeunganishwa na Nida, mifuko ya hifadhi ya jamii, mifumo ya benki na Wezesha Portal, hatua inayorahisisha utambuzi wa wafanyabiashara na upatikanaji wa mikopo, huduma za kifedha, masoko na fursa nyingine za kiuchumi.

Aidha, wizara imetoa mafunzo kwa washiriki 139 kutoka wizara, mikoa, mamlaka za serikali za mitaa na viongozi wa wafanyabiashara ili kuimarisha usimamizi wa mfumo wa utambuzi na usajili wa wafanyabiashara ndogondogo.

Katika kipindi cha Julai 2025 hadi Aprili 2026, wizara ilipokea Sh10.5 bilioni kwa ajili ya mikopo ya wafanyabiashara ndogondogo. Fedha hizo zimefanya kiasi kilichopokelewa kufikia Sh18.5 bilioni tangu Januari 2025, ambapo tayari Sh17.9 bilioni zimetolewa kwa wanufaika 8,426 kupitia Benki ya NMB.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *