Dar es Salaam. Simulizi za wafanyabiashara wanaoanza kwa matumaini makubwa na kuishia kufunga biashara zao zimekuwa za kawaida nchini Tanzania.
Wafanyabiashara wadogo wengi wameendelea kusuasua huku biashara zao zikishindwa kufikia mafanikio makubwa kutokana na changamoto mbalimbali zinazowakabili katika safari ya kujenga na kukuza mitaji yao.
Wataalamu wa uchumi wanataja biashara za wajasirimali kama mama lishe, wauza bidhaa mitandaoni, wasafirishaji wa mazao, mafundi, wamiliki wa maduka madogo, wasindikaji wa mazao ya kilimo hadi viwanda vidogo vya uzalishaji, biashara ndogo na za kati (SMEs) na sekta binafsi kwa ujumla wake ndizo zinazotajwa kubeba sehemu kubwa ya ajira na shughuli za kiuchumi nchini.
Hata hivyo, nyingi zimeendelea kuyumba huku wafanyabiashara wake wakilalamikia ukosefu wa mitaji, ugumu wa kupata mikopo, riba kubwa pamoja na baadhi ya kodi na tozo wanazodai zimekuwa kikwazo kwa ukuaji wa biashara zao.
Wadau wakishiriki katika Jukwaa la Uwekezaji wenye Athari chanya Tanzania (Tanzania Impact Investment Forum – TIIF 2026) lililoandaliwa na Ubalozi wa Uswisi kwa kushirikiana na wadau jijini Dar es Salaam, Jumatatu June 1, 2026
Wasiwasi huo unaakisiwa pia na matokeo ya utafiti wa Tanzania Investment and Consultant Group Limited (TICGL) unaoonyesha kati ya asilimia 60 hadi 70 ya biashara changa nchini hushindwa kuendelea ndani ya miaka mitatu ya kwanza tangu kuanzishwa kwake kutokana na changamoto mbalimbali za kifedha na kimazingira.
Hayo yametawala mjadala katika Kongamano la Uwekezaji wenye athari chanya Tanzania (Tanzania Impact Investment Forum -TIIF) 2026 lililoanza leo Jumatatu Juni 1, 2026 jijini Dar es Salaam, ambapo wawekezaji, wafadhili, taasisi za fedha, viongozi wa serikali na wafanyabiashara wamekutana kujadili namna ya kuziba pengo kati ya biashara zenye ndoto za kukua na vyanzo vya mitaji vinavyoweza kuzisaidia kufika huko.
Pengo la mitaji na mazingira ya biashara
Kongamano hilo la siku tatu lililoandaliwa na Ubalozi wa Uswisi nchini Tanzania kwa ushirikiano na wadau mbalimbali wa maendeleo na uwekezaji, limebeba kaulimbiu isemayo, “Kufungua Mitaji kwa Ukuaji: Kuwekeza katika SMEs zenye Athari Kubwa na Miradi ya Mabadiliko,” likilenga kuibua fursa ya ukuaji wa biashara nchini na kuchochea Uwekezaji wenye athari chanya kwa jamii.
Watoa mada katika Jukwaa la Uwekezaji wenye Athari chanya Tanzania (Tanzania Impact Investment Forum – TIIF 2026) wakiwa katika picha ya pamoja.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kongamano hilo, Balozi wa Uswisi nchini Tanzania, Nicole Providoli, amesema changamoto kubwa inayowakabili wafanyabiashara wengi wadogo si ukosefu wa mawazo ya biashara pekee, bali ugumu wa kufikia fursa za kifedha zinazoweza kuwasaidia kukuza biashara zao.
“Changamoto yao kubwa ni kufikia fursa za kifedha, jukwaa la leo, limewaleta pamoja wadau wote muhimu katika kuwezesha kuziba pengo hilo,” amesema.
Amesema kwa muda mrefu Uswisi imekuwa ikiunga mkono jitihada za kukuza biashara ndogo na ubunifu nchini kupitia programu mbalimbali zinazowasaidia wafanyabiashara kupata maarifa, mitandao na mitaji inayohitajika kukuza biashara zao.
Kwa upande wake, Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Marianne Young, amesema umuhimu wa jukwaa hilo unatokana na ukweli kwamba Tanzania ni taifa lenye idadi kubwa ya vijana wanaohitaji fursa za kiuchumi na ajira.
“Swali ni namna gani Tanzania itakavyoweza kutumia fursa hiyo katika kujenga uchumi endelevu. Ubalozi wa Uingereza utaendelea kushirikiana na Tanzania katika eneo hilo,” amesema.
Amesema ushirikiano kati ya serikali, wawekezaji na sekta binafsi ni muhimu katika kuhakikisha biashara ndogo zinakuwa injini ya ukuaji wa uchumi badala ya kubaki katika hatua ya kusuasua kwa muda mrefu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Stanbic Tanzania, Manzi Rwegasira, akizungumza wakati wa ufunguzi wa Jukwaa la Uwekezaji wenye Athari chanya Tanzania (Tanzania Impact Investment Forum – TIIF 2026) lililofanyika jijini Dar es Salaam leo Jumatatu Juni 1, 2026, likiwakutanisha wawekezaji wa ndani na nje kujadili fursa za uwekezaji wenye matokeo chanya kwa jamii na uchumi.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Stanbic Tanzania, Manzi Rwegasira, amesema mafanikio ya uwekezaji wenye matokeo chanya hayawezi kupatikana kwa upande mmoja pekee, akitoa wito kwa wadau kushirikiana katika kufikia mafanikio.
“Kwa Serikali, jambo la msingi katika kufikia mafanikio si kutoa fedha, bali kujenga mazingira wezeshi kwa wadau kushiriki kikamilifu katika shughuli za uwekezaji,” amesema.
Kauli yake imeelekeza mjadala kwenye hoja ambayo imekuwa ikitajwa mara kwa mara na wafanyabiashara; kwamba pamoja na umuhimu wa mitaji, mazingira ya biashara nayo yana nafasi kubwa katika kuamua kama biashara itakua au itakufa.
Kodi, riba na maarifa ya biashara
Hoja hiyo imefafanuliwa zaidi na mchumi na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Abel Kinyondo, ambaye alipozungumza na Mwananchi kuhusu changamoto za kibiashara nchini amesema mazingira ya biashara, kodi na tozo bado ni sehemu ya vikwazo vinavyokwamisha ukuaji wa biashara nyingi nchini.
“Watu wengi wameajiriwa na sekta binafsi, ili kuchochea zisife, Serikali inapaswa kuwekeza katika mazingira wezeshi ili biashara ziweze kukua,” amesema.
Mbali na kodi na tozo, Profesa Kinyondo amegusia changamoto ya riba za mikopo ya benki za biashara ambazo amesema bado ni kubwa ikilinganishwa na baadhi ya nchi nyingine.
“Serikali kupitia Benki Kuu na benki za biashara zinapaswa kuangalia suala la riba ya mikopo ya wafanyabiashara, kwani riba zetu hapa nchini ni kubwa ukilinganisha na mataifa mengine hali inayoathiri ukuaji wa biashara,” amesema.
Amefafanua gharama kubwa za kukopa zimeendelea kuwafanya wafanyabiashara wengi kushindwa kupanua biashara zao hata pale wanapokuwa na soko na fursa za kukua.
Lakini si changamoto zote zinatokana na mazingira ya nje. Profesa Kinyondo amesema baadhi ya biashara zimekuwa zikishindwa kwa sababu ya maamuzi ya wamiliki wake.
“Badala yake, watu wafanye biashara kwa kuielewa, kujiandaa na kujua changamoto zake ili zisije kuibuka baadaye na kufanya biashara isiendelee,” amesema akionya dhidi ya tabia ya kuingia kwenye biashara kwa kufuata mkumbo baada ya kuona wengine wamefanikiwa.
Balozi wa Uswisi nchini Tanzania, Nicole Providoli (katikati) na Balozi wa Uingereza Tanzania, Marianne Young (kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Stanbic Tanzania, Manzi Rwegasira, wakati wa Jukwaa la Uwekezaji wenye Athari chanya Tanzania (Tanzania Impact Investment Forum – TIIF 2026) lililofanyika jijini Dar es Salaam leo Jumatatu Juni 1, 2026.
Kwa upande wa wafanyabiashara, Mkurugenzi Mwanzilishi wa kampuni ya GBRI, Hadija Jabiri, amesema changamoto si kwamba fursa za fedha hazipo, bali wengi hawajui namna ya kuzifikia na kuzitumia.
“Siku hizi majukwaa mengi wanasema mitaji ipo ila changamoto wafanyabiashara wengi hatujui jinsi ya kunufaika na fursa zilizopo,” amesema.
Hadija, ambaye kampuni yake inajishughulisha na ununuzi, usafirishaji wa mazao na uzalishaji wa mafuta ya parachichi yanayouzwa katika masoko ya Ulaya, amesema mafanikio ya biashara yake yametokana na kupata msaada wa kitaalamu na fursa za uwezeshaji kutoka kwa wadau mbalimbali.
Akifafanua maudhui ya jukwaa hilo, Balozi Nicole amesema, katika kutafuta majibu ya changamoto hizo ndipo Uswisi imeibua jukwaa la TIIF 2026 ikikusudia kuwakutanisha zaidi ya washiriki 300, wakiwemo wawekezaji wa ndani na nje, taasisi za fedha za maendeleo, wafadhili na biashara ndogo na za kati, ili kujadili namna ya kuongeza upatikanaji wa mitaji, kutumia mifumo bunifu ya ufadhili, kukuza uwekezaji wa kijani na kuimarisha matumizi ya teknolojia katika biashara.
Kwa wengi waliohudhuria kongamano hilo, mjadala umekuwa si tu kuhusu upatikanaji wa mitaji kwa wafanyabiashara, bali mjadala mpana wa wadau kuhusu namna ya kuziba pengo kati ya wafanyabiashara wanaohitaji kukua na mifumo inayoweza kuwafikisha kwenye malengo hayo.
Hayo yanajiri kuku takwimu za TICGL zikionyesha kuwa biashara sita hadi saba kati ya kila biashara 10 changa hufa kabla ya kutimiza miaka mitatu, hatua inayofanya majibu ya changamoto hizo kuwa muhimu zaidi katika kuamua hatma ya maelfu ya wafanyabiashara wanaoendelea kupambana ili wafanikiwe kuvuka daraja kuelekea uchumi wanaoukusudia.