Dodoma. Wabunge wameitaka Serikali kusimamia maadili ikiwemo utoaji elimu ya haki, kuliko ambavyo baadhi ya maeneo wanaume wameachwa nyuma huku wanawake wakionekana kupendelewa.
Kauli hiyo imetolewa na wabunge leo Jumatatu Juni Mosi 2026 wakati wakichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu iliyowasilishwa na Waziri wake, Dk Doroth Gwajima.
Mbunge wa Katavi, Thomas Maganga amesema bado kuna kazi ya kufanya kwani eneo la maadili limekuwa na changamoto kubwa huku akilalamikia udhaifu wa sheria katika kuwashughulikia wanaokiuka maadili.
Maganga amesema kama hakutakuwa na utashi wa kisheria na kutoa nafasi kwa vyombo kusimamia maadili, kuna uwezekano mkubwa Taifa likakosa nguvu kazi hasa kwa vijana wa kiume akitumia maneno makali kuwa, Wizara ya Viwanda ijiandae kutengeneza ‘pampasi’.
Mbunge wa Katavi, Thomas Maganga, akichangia mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu kwa mwaka wa fedha 2026/2027, bungeni jijini Dodoma. Picha na Said Khamis.
Mbunge huyo amependekeza iundwe taasisi ya kushughulikia wanaokiuka maadili kama ilivyo kwa taasisi ya kuzuia na kupambana na dawa za kulevya lakini akasema bila kufanya hivyo itakuwa ni kazi ya bure.
Mbunge huyo ametoa mchango wake kwa kutumia vitabu vya dini, ambavyo alikuwa navyo mkononi akieleza kuwa vinapinga vitendo vya kukiuka maadili vinavyofanywa na vijana wa kiume na Mungu ameweka laana kwenye eneo hilo.
Kwa upande wake Mbunge wa Kigoma Mjini, Baba Levo amesema baadhi ya mafunzo yanayotolewa katika kuwajengea uwezo wanawake, yanawajenga kama watu wanaotakiwa kushindana na wanaume na hivyo kuleta tatizo kwa upande wa pili.
Baba Levo amesema baadhi ya wanaume wanapitia kwenye shida nyingi ikiwemo utunzaji wa mimba hadi watoto wanafikia umri wa miaka 10 lakini mwisho wake huambiwa siyo watoto wao, wanawake kunywa pombe za watu na kisha kuwakimbia na wengine kutumiwa nauli lakini hawatokei.
“Lakini wanawake wakipata pesa huota kiburi na kuanza kuwadharau wanaume ambao wanakuwa nyuma kwenye kipato, na hili suala la mwanamke kwenda kumrekodi kiongozi nalo ni janga kubwa hata linapelekea ukatili,” amesema Baba Levo.
Mbunge wa Viti Maalum (wenye ulemavu) Nasriya Nasir Ali, amesema licha ya juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali, lakini mapambano dhidi ya ukatili kwa wanawake na watoto yanapaswa kupewa msukumo wa pamoja, kuliko ilivyo sasa ambapo ameachiwa Waziri Dk Gwajima peke yake.
Mbunge wa Viti Maalum, Nasriya Nasir Ali, akizungumza wakati akichangia mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu kwa mwaka wa fedha 2026/2027, bungeni jijini Dodoma. Picha na Said Khamis.
Nasriya amesema katika baadhi ya maeneo bado kuna unyanyapaa na uonevu hasa kundi la wanawake wenye ulemavu ambao mara nyingi hawana mawasiliano ya moja kwa moja na watoa huduma, hivyo akaomba Watanzania kuunganisha nguvu na kuwapinga watu wa aina hiyo.