NI kawaida bendera kushusha usiku, lakini leo, Jumanne itakuwa tofauti wakati bendera ya Tanzania itapepea usiku timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17, Serengeti Boys itashuka dimbani kuivaa Senegal katika fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika U-17 Saa 4:00 usiku kwenye Uwanja waMoulay El Hassan jijini Rabat, Morocco.
Serengeti Boys inashuka uwanjani ikiwa imebeba matumaini ya soka la Tanzania katika jukwaa kubwa zaidi la soka la vijana barani, kizuizu pekee kuifikia ndoto hiyo ni Senegal mabingwa wa zamani wa mashindano hayo.
Mashindano ya mwaka huu yameleta mshangao mwingi, lakini hakuna uliovutia zaidi kuliko safari ya ajabu ya Serengeti Boys kufika fainali kwa mara ya kwanza katika historia yao. Tanzania ilifika hatua hiyo baada ya kuiondoa Misri U-17 kwa mikwaju ya penalti katika nusu fainali, kufuatia ushindi mwingine wa penalti dhidi ya Algeria U-17 katika robo fainali.
Baada ya kumaliza kileleni mwa kundi lao na kuvuka mechi mbili ngumu za hatua ya mtoano, vijana hao wameonyesha uimara, uthubutu na kujiamini kuliko umri wao.
Ushindi dhidi ya Senegal katika fainali utakuwa mafanikio makubwa zaidi kuwahi kupatikana na soka la Tanzania.
Jambo la muhimu zaidi ni kuwa hakuna timu yoyote ya taifa ya Tanzania iliyowahi kushinda taji la AFCON. Hata Taifa Stars bado inasaka ubingwa wake wa kwanza wa Afrika licha ya kushiriki mashindano hayo mara kadhaa. Ndiyo maana fainali hii zinauzito mkubwa kwa taifa zima.
Kutwaa ubingwa wa U-17 AFCON kutakuwa ushahidi kuwa uwekezaji katika maendeleo ya soka la vijana nchini Tanzania unaanza kuzaa matunda. Pia utatoa hamasa kubwa kwa taifa linalojiandaa kuwa mwenyeji mwenza wa PAMOJA AFCON2027 na majirani zake Kenya na Uganda.
Mafanikio ya Tanzania pia yanaonyesha ukuaji wa soka la Afrika Mashariki kwa ujumla. Kwa mataifa ya Tanzania, Uganda na Kenya yameongeza uwekezaji katika soka la vijana, huku klabu za ukanda huo zikianza kufanya vizuri zaidi katika mashindano ya CAF.
Katika ngazi za vijana na wakubwa, mataifa yanayoibukia sasa yanaanza kutoa ushindani mkubwa dhidi ya vigogo wa jadi wa soka la Afrika. Bila kujali matokeo ya fainali, Tanzania tayari imeandika historia. Lakini kuinua kombe hilo kutageuza safari hii ya kuvutia kuwa tukio la mabadiliko makubwa kwa soka la taifa.
Ubingwa huo utakuwa taji la kwanza kubwa la soka la bara kwa Tanzania, utaongeza imani kuelekea AFCON 2027, na kuthibitisha kuwa Tanzania sasa ni sehemu ya nguvu mpya zinazochipukia soka la Afrika.