WAKATI Simba ikielekea kumalizia hatua za mchakato wa mabadilko ya uendeshaji, uongozi wa klabu hiyo umeonyesha ukuaji mkubwa wa mapato ukisema mishahara ya wachezaji wa timu hiyo kwa sasa inagharimu Sh700 milioni kwa mwezi.
Simba imekuwa na mafanikio makubwa kipindi cha karibuni ambapo imefanikiwa kufika hatua ya robo fainali ya michuano ya klabu ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) mara kadhaa na fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika mara moja, huku pia ikiwania ubingwa wa Ligi Kuu Bara.
Aliyetoa mwelekeo huo ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Crescentius Magori, akisema ndani ya miaka tisa kuanzia 2017 ambao safari ya mchakato wa mabadiliko ilianza Simba imetoka kwenye bajeti ya Sh70 milioni kwa mwezi na kufikia Sh700 milioni kwa mishahara.
Magori ameliambia Mwanaspoti kuwa bajeti hiyo ndio eneo lililochangia mafanikio makubwa Simba ambapo iliweza kuwahudumia wachezaji wenye uwezo mkubwa ambao waliwapandisha wekundu hao kuwa klabu yenye mafanikio na ubora Afrika.
Bosi huyo ambaye amepewa jina la ‘General’ na mashabiki, amesema ndani ya kipindi hicho cha miaka tisa Simba imetoka kuwa na bajeti isiyofika Sh2 bilioni kwa mwaka mpaka sasa inatumia bajeti ya Sh25 bilioni kwa mwaka mmoja kwa uendeshaji kwa ujumla.
“Nakumbuka wakati tunaanza safari hii ya mabadiliko mwaka 2017 bajeti ya Simba ilikuwa haifiki bilioni mbili na mishahara ya wachezaji wakati huo ilikuwa kwenye milioni 60 mpaka 70 hapo hazikuwa fedha nyingi sana,” amesema.
“Sasa unazungumza ni miaka tisa tumetoka kwenye bajeti ya mishahara ya Sh70 milioni kwa mwezi mpaka sasa tunalipa karibu kabisa na Sh700 milioni kwa mwezi.
“Sasa ukipiga asilimia ya ukuaji unaweza kuona tumekua kwa haraka sana ndani ya kipindi cha miaka tisa na ni kipindi ambacho tulikuwa bado tunapitia nyakati za ndani ya safari ya mabadiliko kwa sababu haya mabadiliko ya Simba ni mageni.
“Hakuna mtu ambaye alikuwa anayajua masuala ya mabadiliko kwamba hii tunakwendaje. Ilikuwa kama shamba darasa kwamba klabu ya wanachama imeamua itamiliki timu yao kupitia kwa hisa (wanachama) wabakie na asilimia 51 na mwekezaji awe na 49.
“Ni kitu ambacho kimechukua muda mrefu na hatimaye sasa tunakwenda kwenye ukamilishaji. Baada ya kupitisha katiba mwezi Januari sasa tunakwenda kuyakamilisha mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji. “Pamoja na kwamba tulikuwa kwenye safari na hatujakamilisha ndani ya kipindi hicho tumeweza kukua kwa kasi ya ajabu sana.’’
Ingawa Magori hakuwataja wachezaji wanaochukua mishahara mikubwa ndani ya kikosi hicho, lakini Mwanaspoti linafahamu kwamba baadhi ya wachezaji wanaotajwa kuvuna mishahara mikubwa ni pamoja na mabeki Rushine De Reuck, Ismael Toure; viungo Neo Maema, Clatous Chama, Lebasse Gueye, Ellie Mpanzu na mshambuliaji Seleman Mwalimu ambaye yupo klabuni hapo kwa mkopo.
Magori pia alieleza kwamba wakati mchakato huo wa mabadiliko ukielekea ukingoni Simba itakwenda kuvuna fedha nyingi kupitia mchakato wa kuanza kusajili wanachama na kwamba klabu hiyo itakwenda kutoa kadi za kisasa zaidi, zitakazounganishwa na taasisi mbalimbali za kutoa huduma za kifedha.
“Wakati zoezi hili linakwenda kukamilika tunategemea sasa maana nafikiri kuanzia mwaka 2017 hatukuwahi kutoa kadi za wanachama kwa sababu tulikuwa kwenye kipindi cha mpito… sasa tunakwenda kutoa kadi za wanachama.
“Tutakwenda kutoa kadi za kisasa zaidi za wanachama. Dunia sasa ipo kwenye hatua kubwa ya teknolojia. Kadi zetu zitamwezesha mwanachama wetu kuitumia kwenye matumizi mbalimbali ya huduma za kifedha na zitaunganishwa kila mwanachama na taasisi anayotaka. Akitumia kwenye eneo lolote katika malipo Simba pia itaingiza fedha,” amesema mwenyekiti huyo.