Babati. Wananchi wa Mkoa wa Manyara sasa wameondokana na adha ya kusafiri kwenda mikoa mingine kutafuta huduma ya kusafisha figo (dialysis), baada ya huduma hiyo kuanzishwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara kwa uwekezaji wa Sh300 milioni.

Hatua hiyo imeelezwa kuwa mkombozi kwa wagonjwa waliokuwa wakilazimika kusafiri umbali mrefu na kubeba gharama kubwa za matibabu na usafiri ili kupata huduma hiyo muhimu.

Mbali na huduma ya dialysis, uboreshaji wa miundombinu katika hospitali hiyo umehusisha pia ujenzi wa majengo mawili ya huduma ya dharura (emergency) na chumba cha wagonjwa mahututi (ICU), hatua iliyoongeza uwezo wa hospitali kutoa huduma za kibingwa.

Hayo yamebainishwa leo Jumanne Juni 2, 2026 na Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, alipokuwa akizungumza wakati wa ziara ya Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi, aliyefanya ukaguzi wa miradi ya afya katika hospitali hiyo.

Sendiga amesema kuanzishwa kwa huduma ya dialysis ni hatua kubwa iliyowaletea nafuu wananchi wa mkoa huo, ambao awali walilazimika kwenda mikoa ya mbali kupata huduma hiyo.

“Huduma ya kusafisha figo ambayo ilikuwa haijawahi kutolewa katika mkoa huu ilianza mwishoni mwa mwaka jana baada ya Serikali kutoa Sh300 milioni. Wananchi walikuwa wakipata changamoto kubwa ya kusafiri umbali mrefu, lakini sasa wanapata huduma hapa hapa Manyara,” amesema Sendiga.

Amesema huduma hiyo imepunguza kwa kiasi kikubwa mzigo wa gharama kwa wagonjwa na familia zao, pamoja na kuimarisha upatikanaji wa huduma kwa wakati.

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara, Dk. Yesige Mutajwaa, amesema ujenzi wa majengo ya ICU na huduma za dharura ulitekelezwa kwa awamu mbili tangu mwaka 2021 kwa gharama ya zaidi ya Sh1.6 bilioni kutoka Serikali Kuu na fedha za ndani ya hospitali.

Amesema uwekezaji huo umeongeza uwezo wa hospitali kutoa huduma za mama na mtoto, wagonjwa mahututi pamoja na majeruhi wa ajali za barabarani.

“Tumekuwa na changamoto kubwa ya ajali za barabarani, lakini majengo haya yameongeza uwezo wa kutoa huduma za haraka na kuokoa maisha ya wagonjwa wengi,” amesema.

Ameongeza kuwa maboresho hayo yamepunguza rufaa za wagonjwa kwenda hospitali za mbali ikiwemo Hospitali ya KCMC mkoani Kilimanjaro.

Kwa upande wake, Kihongosi amesema maboresho ya miundombinu ya afya ni ushahidi wa utekelezaji wa Ilani ya CCM na dhamira ya Serikali ya kuboresha huduma kwa wananchi.

Amesema huduma hizo zimeleta mabadiliko makubwa kwa wakazi wa Manyara na maeneo jirani, kwa kuwa sasa huduma muhimu zinapatikana karibu na wananchi.

“Zamani wagonjwa walikuwa wakisafirishwa mbali, lakini sasa huduma muhimu zinapatikana hapa hapa. Hii ndiyo falsafa ya kazi na utu kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kwa wakati,” amesema.

Ameitaka jamii kulinda miundombinu ya afya iliyojengwa, akisema ni rasilimali muhimu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *