
Tony Addison ni mwanazuoni na mtafiti wa Chuo Kikuu cha Umoja wa Mataifa (UNU), ambacho kipo Jaan.
Addison anafanya kazi za utafiti kupitia Taasisi ya Ulimwengu kwa ajili ya Utafiti wa Maendeleo ya Uchumi (UNU-WIDER).
Nimesoma maandiko ya Addison kuhusu utafiti wake katika nchi 44 zilizopata kuwa na migogoro ya kisiasa.
Kuanzia Colombia, Guatemala, Shirikisho la Yugoslavia, Zimbabwe, Ivory Coast, Guinea Bissau, Rwanda, Angola, Cambodia, Timor Mashariki, Kosovo, Msumbiji, Eritrea, Ethiopia, Somalia, na maeneo mengine. Siri kubwa ya migogoro ni fedha.
Andiko la kwanza lenye kichwa “Conflict and Financial Reconstruction” – “Mgogoro na Ujenzi Mpya Kifedha,” lililochapwa kwenye tovuti ya UNU-WIDER, Addison anaeleza kuwa udhibiti wa fedha husaidia amani kupatikana haraka. Pande zinazosigana zinapokosa rasilimali, huwa rahisi kuketi mezani na kujadili mapatano ya amani.
Andiko lingine lina utambulisho “Finance in Conflict and Reconstruction” – “Ufadhili kwenye Mgogoro na Ujenzi Mpya.”
Addison ameshirikiana na watafiti wengine, Philippe Le Billon na Mansoob Murshed. Hapa wanaeleza namna vikundi vya uasi na wanaharakati wanavyopata fedha ndani na nje ya nchi.
Jumuiya za kimataifa hutoa fedha kufadhili vikundi vya uasi na wanaharakati. Hoja hii haiishii kwa Addison, Billon na Murshed, bali pia inaongezewa nguvu na tuhuma ambazo Rais wa Kenya, William Ruto alizitoa Julai 2024, dhidi ya taasisi ya misaada ya kifedha ya Marekani, Ford Foundation. Ruto alisema taasisi hiyo ndiyo iliyokuwa inafadhili migogoro Kenya.
Mapato mengine kwa wanaharakati na waasi hutoka kwa raia wanaoishi nje ya nchi zao (diaspora), ambao huwa na masilahi kwenye migogoro husika.
Wakati mwingine, michezo michafu huchezwa kwenye taasisi za kifedha za ndani ili kufadhili pande zinazosigana kwenye migogoro ya kisiasa.
Addison, Billon na Murshed, wamekwenda ndani zaidi na kuweka wazi kuwa makundi ya fedha chafu, hasa wafanyabishara wa dawa za kulevya, wasafirishaji haramu wa binadamu, magenge ya kimafia na kadhalika, huingiza fedha kwenye migogoro ya kisiasa, hivyo kusababisha amani iwe vigumu kupatikana. Msingi wa hoja hapa ni fedha. Shughuli za kisiasa na harakati, zinapopewa manufaa ya kifedha, hali huwa mbaya.
Mivutano huwa haiishi. Mikutano inaweza kufanyika lakini suluhu isipatikane. Maana kila mmoja atazingatia yale anayopata na atakayokosa pale amani inapotawala na migogoro kuisha.
Mambo ya Oktoba 29, 2025, pamoja na manung’uniko yaliyokuwapo, kukosekana usawa kwenye uchaguzi, rushwa na tatizo la ajira, lakini pia kulikuwa na presha kubwa kutoka kwa Watanzania wanaoishi nje ya nchi. Yalikuwepo maneno yaliyozagaa mitandaoni kuwa kuna taasisi za kimataifa zilikuwa zinawafadhili wanaharakati waliokuwa mstari wa mbele kuhamasisha watu kuingia barabarani kuzuia uchaguzi.
Ipo hali ilikuwa inatisha. Watanzania kukimbia nchi yao na kwenda kuishi Kenya na nchi nyingine za ughaibuni, kutwa wanashinda mitandaoni.
Ufadhili ulipatikana wapi? Kodi za nyumba, chakula na mavazi, pamoja na intaneti. Hili lilileta wasiwasi kwa kila ambaye alikuwa anafuatilia kwa karibu.
Fedha si tatizo kwa wapinzani wa kisiasa na wanaharakati peke yao, hata walio kwenye mamlaka ni shida. Unakuta serikali iliyopo madarakani, ndani kwa ndani, kunakuwa na uchochezi wa migogoro kuendelea kwa sababu kuna watu ndani ya mfumo wananufaika kifedha pale hali ya nchi inapokosa utulivu.
Yaliyotokea Oktoba 29, yanafahamika. Vifo vya watu 518 ambao hapo kuna raia na askari. Uharibifu wa miundombinu na mali. Wizi ulitokea. Waliouawa ni Watanzania, walioibiwa na kuharibiwa mali zao ni Watanzania. Hata miundombinu na mali za umma zilizoporwa na kuharibiwa, ni za Watanzania.
Mtu mwenye moyo wa Kitanzania, ambaye anafanya mambo yake bila kuwa chini ya ushawishi, hawezi kukubali yaliyotokea Oktoba 29, yajirudie kwa mara nyingine.
Maana ameshaona madhara yake. Njia pekee ya kuzuia yaliyojiri yasijirudie ni mazungumzo, siyo kutumia njia zilezile zilizoleta maafa na uharibifu mkubwa.
Adui wa maisha ya Mtanzania anaweza kuwa fedha. Pande mbili zenye masilahi ya kifedha, zinaposuguana, haziwezi kutafakari na kujisahihisha. Kama njia ileile waliyoitumia bado inawapa fedha, wataendelea nayo. Watahamisha tarehe kutoka Oktoba 29, Desemba 9 na 25, 2025, mpaka Julai 7, 2026.
Kazi kubwa lazima ifanyike kubaini mitego ya kifedha. Je, wanaotaka ya Oktoba 29 yajirudie Julai 7, wanapata ufadhili wapi? Vipi upande wa dola, wasiotaka kusikiliza malalamiko ya upande wa pili na kushauri vizuri ili nchi iwe salama, badala yake wanachochea makabiliano ya kidola, nyuma yao wanavuna nini?
Somo ni moja, endapo mirija ya fedha chafu itazibwa, itakuwa rahisi kuwaona wapinzani halisi na wanaharakati wenye utashi binafsi. Hata ndani ya dola, kutakuwa na uamuzi bora ambao utawezesha kuwaleta wapinzani na wanaharakati pamoja ili kuijenga kesho nzuri ya Tanzania.
Vinginevyo, Tanzania hii inayoonekana imara, inaweza kugeuka Somalia. Usalama utakosekana. Magenge machafu ndiyo yatakuwa yanaamua nchi iende vipi. Serikali kuu itapoteza meno.
Ni muhimu sana kuiepusha nchi kwenda kwenye njia mbaya. Mahali nchi ilipo, ni mwanzo wa uelekeo mbaya.
Kesho njema itajengwa na Watanzania wanaotofautiana na kusuguana kwa hoja kuhusu hatima ya nchi yao. Wanaotambua kuwa kila upande una malengo mema na nchi. Wasioendekeza masilahi ya kifedha na tamaa ya madaraka, hao ndiyo Watanzania wa kweli zaidi.
Wanaotambua kwamba Tanzania haiishii kwenye tarakimu za uhai wao, bali itakuwepo vizazi vingi vijavyo. Watanzania wajao wanatakiwa kuikuta nchi ikiwa nzuri na salama kuishi.
Utanzania ukitamalaki, itakuwa wazi kwamba waliopo madarakani ni Watanzania, vilevile wapinzani na wanaharakati ni Watanzania. Hakutakuwa na hoja za ukombozi wa nchi, bali michakato ya kubadilisha viongozi.
Maana Tanzania ni nchi huru. Haijavamiwa wala kutekwa. Kama kuna makosa yanafanywa na wenye madaraka, basi ni makosa ya Watanzania kwa Watanzania.