Lindi/Mtwara. Wakati wananchi wa Nyengedi wakiendelea kusubiri fidia na hatima ya ardhi yao, uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa changamoto za kifedha na kiutendaji ndizo zinatajwa kuwa chanzo cha kusimama kwa mradi huo.

Akizungumzia suala hilo, mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye anakiri kuwapo kwa tatizo hilo, akisema changamoto kubwa ni ukosefu wa fedha za utekelezaji licha ya miradi kutajwa kwenye bajeti.

“Ni kweli hilo jambo lipo lakini mimi kama mbunge sina cha kufanya sababu changamoto kubwa hapa ni Serikali haijaweka fedha licha ya kuainisha katika bajeti yake.

“Ushauri wangu, umtafute Waziri wa Mifugo na Uvuvi, huyu ndiye anaweza kukupa majibu sahihi kwamba wamefikia wapi sababu hata mimi nilijaribu kuzungumza naye tukiwa bungeni juu ya mradi wa Nyengedi lakini hata yeye haufahamu kabisa,” anasema Nape.

Mamlaka zinatambua jambo hilo?

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtama, Yusuf Abdallah Tipu ambaye pia ni Diwani wa Nyengedi, alipotafutwa na Mwananchi juu ya kuzungumzia jambo hilo anasema kuwa hawezi kuzungumzia suala hilo kwa haraka hivyo.

Swali: Hapa kuna mradi wa bwawa la ufugaji samaki na vifaranga wa Nyengedi je umefikia wapi?

Akijibu swali hilo Tipu anasema: “Mimi sina cha kukujibu kwa harakaharaka.”

Mkurugenzi akiri mradi kusuasua

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mtama, Anderson Msumba, anakiri kuufahamu mradi huo huku akisisitiza kwamba hauko chini yao badala yake watafutwe wahusika waliokita kambi mjini Mtwara.

Swali: Mkuu kuna mradi upo maeneno ya Nyengedi wa ufugaji wa bwawa la samaki nilikuwa nataka kufahamu umefikia wapi?

“…mmh…ule mradi ni wa wizara kimsingi (Wizara ya Mifugo na Uvuvi) na wenyewe wako Mtwara ofisi yao, ule mradi ulikuwa ni mradi wa kufuga samaki wa maji baridi, wafuge samaki na iwe ni kitalu cha kuotesha mbegu.

Walikuwa na ishu kidogo ya fidia kwenye kujenga ofisi zao na miundombinu yao ndio walikuwa hawaja-clear (kumaliza) lakini mradi upo ila tu suala la fidia ndilo linasuasua, sisi kwetu bado hawajatukabidhi,” anasema Msumba.

Msimamizi wa mradi

Wakati wakubwa hao wakiendelea kutupina mpira juu ya kukwama kwa mradi huo wa Nyengedi hadi sasa,

Robart Nicholaus anayesimamia kanda hiyo ya kusini anakiri kuwapo kwa mkwamo katika utekelezaji wa mradi huo huku akisisitiza zaidi zitafutwe ngazi za juu kwa maana ya wizara yenyewe na kwamba licha ya yeye kuwa msimamizi wa mradi huo,  hana mamlaka ya kuzungumza na vyombo vya habari bila idhini hususan juu ya mradi huo.

“Sasa unajua brother (kaka) iko hivi, kiprotocal mimi ni Zone Incharge lakini protocal ya kutoa maelezo ya Serikali lazima ifuatwe.

“Na ukweli ni kwamba katika mambo kama haya yanahusu wizara mimi ni mmoja wapo wa waajiriwa wa wizara sawa, na mimi ni mkuu wa kanda ya kusini kwenye jambo hilo, sasa ninapotoa suala linalohusu wizara lazima protocal ifuatwe kwa sababu mimi siyo msemaji wa moja kwa moja vinginevyo naweza kusema jambo linalohusi wizara kama nimekasimiwa kufanya hivyo, kutoka kwa katibu mkuu ambaye ndiye bosi wangu au mkurugenzi wa idara yangu,” anasema Nicholaus.

Hata hivyo, Nicholaus anakiri kuwapo kwa mradi huo na kuthibitisha kuwapo kwa ucheleweshaji huku akisema kuwa kuhusu sababu hawezi kueleza.

“Sasa nasikitika, sawa huo mradi upo, huo mradi upo sometime kama kunadelay (kusuasua) sababu ni nini siwezi kueleza kwa sababu ni suala ambalo ingekuwa vizuri kama ungeenda wizarani ukaweza kupata maelezo angalau kidogo kwa msemaji wa wizara, mimi nafikiri hataa ukienda kwa mkurugenzi wa idara hii inayohusika na mradi huo kuna maelekezo atakupa lakini ni dhahiri kuwa na yeye atakuelekeza kwa bosi mkubwa sababu yeye ndiye kila kitu,” anasema na kuongeza:

“Kwa hiyo inakuwa vigumu kwangu kukupa taarifa za namna hiyo kiprotocal na ni utaratibu wa utumishi wa Serikali, hivyo kama kuna maelekezo nitapewa na kuna mawasiliano ikiwapo nyaraka basi nitakusaidia lakini hata maelezo ninayo jua kuhusu mradi kiplotocal kuna mengine siwezi kuyasemea, kwa hiyo uwafikie wizarani Dodoma wataweza kukusaidia,” anasema Nicholaus.

Mwananchi pia ilimtafuta Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Agnes Meena juu ya kusuasua kwa mradi wa Ruvula mkoani Mtwala na kukwama kwa mradi wa Nyengedi, anadai  changamoto kubwa ni kukosekana kwa bajeti na kwamba fedha ikipatikana miradi hiyo itatekelezwa.

“Unajua mradi wa Serikali ukiwa umesimama siyo kwamba umeachwa badala yake ni fedha bado hakuna, hivyo miradi yote miwili ya Ruvula kule Mtwara na Nyengedi Lindi imesimama sababu ya kukosa fedha, fedha itakapopatikana miradi yote itatekelezwa kama ilivyopangwa,” anasema Meena.

Akijibu juu ya miradi hiyo kutengewa fedha kila mwaka kwenye bajeti ya wizara lakini haitekelezwi, Meena anasema kuwa kutengewa fedha ni jambo moja lakini fedha kuwepo ni jambo jingine na kwamba kuna miradi mingi na siyo hiyo tu bali kuna miradi mingine.

Mradi wa Ruvula-Mtwara

Kituo cha Ruvula kilichopo umbali wa kilometa 40 kutoka Mtwara Mjini, kilitarajiwa kuwa kitovu cha ukuzaji wa viumbe maji baharini (mariculture), kimeonesha dalili za kuchelewa kukamilika licha ya hatua za awali za ujenzi kufanyika.

Kwani pamoja na Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kujinasibu kuwa mradi huo umekamilika, uhalisia wake unaonesha kwamba bado kuna kazi ya kufanya kuhakikisha mpango huo mkubwa wa uwekezaji unakamilika.

Mathalani, Januari 14, 2024 aliyekuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega alipotembelea mradi huo, aliagiza mradi huo kukamilika haraka ili uweze kuwanufaisha wananchi wa maeneo hayo kupitia miradi mbalimbali ikiwamo biashara ya majongoo bahari ambayo yana fursa kubwa hususan barani Asia.

“Mahitaji ya majongoo bahari, kaa, mwani, kambakochi na mwatiko ni makubwa katika nchi za Asia hasa China, hivyo ni lazima tucheze na fursa tulizonazo ili tuweze kufanikiwa na ndio maana Serikali inatoa elimu kuwawezesha wananchi hususan vijana na kinamama kufanya shughuli hizo ili wauze nje ya nchi wajipatie kipato,” alibainisha Ulega wakati wa ziara yake hiyo.

Hata hivyo, miaka miwili baadaye tangu kufanyika kwa ziara hiyo na kutolewa kwa maelekezo ya kukamilika kwa mradi huo, bado mradi huo umeendelea kusalia vilevile japo una unafuu ikilinganishwa na ule wa Ruvula.

Mwananchi ilifika eneo la mradi huo ulilopo katika Kata ya Msimbati Wilaya ya Mtwara Vijijini na kujionea hali halisi ikiwa kama ilivyoshuhudwa wakati wa ziara ya Waziri Ulega.

Mmoja wa wasimamizi wa mradi huo ambaye hakutaka jina lake litajwe sababu ya kutokuwa na mamlaka ya kuzungumzia mradi huo alisema kuwa mradi huo tayari umekamilika kwa asilimia 99 na kwamba kinachosubiriwa ni mvua(kujaa kwa maji bahari) kwa ajili ya kusukuma maji kuingia kwenye mitambo hiyo na kuanza uzalishaji na utotoleshaji wa vifaranga ikiwamo majongoo bahari.

Anasema mradi huo ambao ulihusisha ujenzi wa majengo na ufungaji wa vifaa vya kisasa, sasa uko mbioni kuanza na kwamba tayari Serikali imeagiza vifaranga kutoka Kinguluwila-Morogoro kwa ajili ya kuanza utekelezaji.

Inatarajiwa kuwa ifikapo mwezi wa nne (Aprili), 2026, mchakato wa utotoleshaji utakuwa umekamilika na kuanza kutoa vifaranga. Shughuli kuu zitakazofanyika katika kituo hiki ni pamoja na utotoleshaji wa vifaranga vya majongoo bahari pamoja na chaza (oysters). Sosi kuu ya maji inayotegemewa katika kituo hicho ni maji ya bahari,” kinaeleza chanzo hicho.

Matumaini ya wananchi kuhusu ujenzi wa vituo vya ufugaji viumbe maji yalikuwa na msingi si tu wa ahadi za viongozi, bali pia ndani ya Fisheries Act (Cap. 279).

Sheria hiyo, kupitia kifungu cha 9(1)(b), inamtaka  mkurugenzi wa uvuvi kuwezesha maendeleo na ukarabati wa miundombinu ya uvuvi pamoja na shughuli zinazohusiana nayo.

Aidha, kifungu cha 9(1)(d) kinaweka bayana wajibu wa Serikali katika kukuza ufugaji wa viumbe maji kwa kutumia teknolojia rahisi na uwekezaji unaoweza kufikiwa na wananchi wengi.

Kwa tafsiri pana, matakwa haya ya kisheria yanaendana moja kwa moja na ahadi ya kujenga vituo vya kisasa vya mafunzo na uzalishaji.

 Hata hivyo, kupita kwa miaka bila utekelezaji wa miradi hiyo, kumeibua maswali ya msingi kuhusu uwajibikaji na usimamizi wa rasilimali za sekta.

Hoja kubwa inaelekezwa kwenye Mfuko wa Maendeleo ya Uvuvi, ulioanzishwa chini ya kifungu cha 29 cha sheria hiyo.

Kwa mujibu wa kifungu cha 30(j), mfuko huo una jukumu la kuchochea maendeleo ya ufugaji viumbe maji pamoja na kuongeza samaki katika vyanzo vya maji vya asili.

Hivyo, kuchelewa au kutotekelezwa kwa miradi inayolenga sekta hiyo kunatia shaka juu ya ufanisi wa matumizi ya mfuko huo, na kwa upana wake kunagusa wajibu wa Waziri mwenye dhamana, ambaye chini ya kifungu cha 3 anapaswa kuhakikisha sera na mipango yote ya wizara inatekelezwa kikamilifu.

Katika ngazi ya utekelezaji, changamoto hii ina athari za moja kwa moja kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Kwa mujibu wa kifungu cha 15(1), mamlaka hizo zina wajibu wa kusimamia na kufuatilia shughuli za ufugaji viumbe maji katika maeneo yao.

Hata hivyo, kukosekana kwa vituo vya mfano na miundombinu iliyokuwa imeahidiwa kunadhoofisha uwezo wao wa kutekeleza jukumu hilo kwa ufanisi. Vilevile, inakuwa vigumu kwa mkurugenzi wa uvuvi kutimiza majukumu yake chini ya kifungu cha 10, ambayo yanahitaji uwepo wa mifumo imara ya usimamizi na maendeleo ya sekta.

Matokeo yake, wafugaji wa samaki wanaendelea kubaki katika mazingira ya sintofahamu, wakishuhudia pengo kubwa kati ya matakwa ya sheria na uhalisia wa utekelezaji wake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *