
Mamilioni ya watalii kutoka duniani kote huitembelea Tanzania kila mwaka wakivutiwa na mandhari yake ya kipekee, wanyamapori wa kuvutia na tamaduni za kale ambazo zimeendelea kuhifadhiwa kwa karne nyingi.
Miongoni mwa maeneo yanayoibeba hadhi hiyo ni Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro, eneo ambalo si tu linajulikana kwa utajiri wa wanyamapori, bali pia kwa urithi wake wa kiutamaduni unaovutia wageni kutoka kila pembe ya dunia.
Kwa mujibu wa Kamishna Mhifadhi wa Hifadhi ya Ngorongoro, Abdul-Razaq Badru akizungumza na UN News Kiswahili amesema, msingi wa utalii endelevu unaanza na uhifadhi endelevu wa mazingira na rasilimali za asili.
Uhifadhi ndiyo msingi wa utalii endelevu
Badru anasema Tanzania imeendelea kuweka mkazo mkubwa katika kusimamia uhifadhi wa mazingira ili kuhakikisha vivutio vya utalii vinaendelea kuwepo kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
“Utalii endelevu unategemea uhifadhi endelevu,” anasema. “Tunafanya juhudi za kuhakikisha uoto wa asili unalindwa, mimea inasimamiwa na wanyama wa aina mbalimbali wanatunzwa kwa sababu uwepo wao ndiyo unaofanya uhifadhi wa asili uwezekane.”
Ngorongoro ni miongoni mwa maeneo machache duniani ambako wageni wanaweza kushuhudia kwa ukaribu baadhi ya wanyama maarufu zaidi duniani, wakiwemo simba, tembo, twiga, nyati na faru. Utajiri huu wa viumbe hai umeifanya Tanzania kuwa moja ya nchi zinazoongoza katika utalii wa wanyamapori barani Afrika.
Ngorongoro: Zaidi ya wanyama pekee
Tofauti na hifadhi nyingi duniani, Ngorongoro si makazi ya wanyamapori pekee. Pia ni nyumbani kwa jamii za watu wa asili ambao wameendelea kuhifadhi tamaduni zao kwa muda mrefu.
Kwa Badru, huo ndio upekee unaoifanya Ngorongoro kuwa eneo la kipekee duniani.
Anasema “Mtalii anayefika Ngorongoro haendi tu kuona wanyama. Anakwenda pia kuona urithi wa kitamaduni wa jamii za Wamasai, Wadatoga, Wahazabe na makundi mengine ambayo yameendelea kuhifadhi mila na desturi zao kwa muda mrefu”.
Anaeleza kuwa tamaduni hizo zimekuwa sehemu muhimu ya kivutio cha utalii, huku mamlaka za hifadhi zikifanya kazi kuhakikisha zinadumu bila kupoteza utambulisho wake wa asili.
Kutafuta uwiano kati ya binadamu na mazingira
Moja ya changamoto kubwa katika hifadhi ya Ngorongoro ni namna ya kusawazisha mahitaji ya uhifadhi na yale ya jamii zinazozunguka au kuishi ndani ya eneo la hifadhi.
Kwa mujibu wa Badru, serikali imeendelea kuweka mikakati ya matumizi bora ya ardhi na rasilimali ili kuhakikisha shughuli za binadamu haziathiri mfumo wa ikolojia unaolipa eneo hilo umaarufu wa kimataifa.
“Ngorongoro ina umahususi wake kwa sababu ni eneo ambalo lina wanyamapori lakini pia lina wakazi wanaoendelea kuishi humo. Hivyo tunasimamia matumizi ya rasilimali kwa namna inayoruhusu uhifadhi kuendelea huku shughuli za kijamii na kiuchumi nazo zikiendelea kwa uwiano unaofaa,” anasema.
Kulinda wanyama walio hatarini kutoweka
Katika kipindi ambacho dunia inakabiliwa na changamoto ya kupungua kwa baadhi ya aina za wanyamapori, Ngorongoro imeendelea kuwa ngome muhimu ya uhifadhi.
Badru anasema kuna shughuli ambazo haziruhusiwi kufanyika ndani ya eneo la hifadhi ili kulinda mfumo wa ikolojia na makazi ya wanyamapori.
“Shughuli za kilimo haziruhusiwi katika eneo la hifadhi kwa sababu tunahitaji kulinda mazingira ya asili yanayowawezesha wanyama kuendelea kuishi,” anafafanua.
Aidha, mamlaka za hifadhi zinasimamia maeneo ya malisho ya mifugo na kuhakikisha hayaingiliani na maeneo muhimu ya wanyamapori. Hatua hiyo imekuwa muhimu katika kulinda vyanzo vya maji vinavyochangia mfumo mkubwa wa ikolojia unaounganisha maeneo ya Serengeti, Grumeti na hata Maasai Mara nchini Kenya.
Urithi wa Afrika kwa dunia Nzima
Kwa miaka mingi, Ngorongoro imeendelea kuwa mfano wa jinsi uhifadhi unavyoweza kwenda sambamba na maendeleo ya binadamu na utalii.
Kwa Badru, mafanikio ya utalii hayawezi kutenganishwa na uwekezaji katika uhifadhi wa mazingira.
“Uhifadhi ni muhimu sana. Tunaweza kuona kwa urahisi manufaa ya utalii, lakini bila kuwa na uhifadhi stahimilivu huwezi kuwa na utalii,” anasisitiza.
Katika dunia inayozidi kukabiliwa na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, ongezeko la watu na shinikizo la matumizi ya rasilimali, ujumbe kutoka Ngorongoro unabaki kuwa wazi, “kulinda mazingira, wanyamapori na urithi wa kitamaduni leo ni kuwekeza katika mustakabali wa utalii na maendeleo ya kesho.”