Uzbekistan. Jitihada za dunia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, upotevu wa bioanuwai na uharibifu wa mazingira zimepata nguvu mpya baada ya Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF) kuidhinisha dola za marekani bilioni 3.9 (Sh9.95 trilioni) kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya mazingira hadi mwaka 2030.

Mbali na kifurushi hicho, Baraza la GEF limeidhinisha dola milioni 232.5 (Sh592.88 bilioni) kwa ajili ya miradi mipya 24 ya mazingira katika nchi 22.

Uamuzi huo ulifikiwa katika mkutano wa 71 wa Baraza la GEF uliofanyika Samarkand, Uzbekistan, leo Jumatano, Juni 03, 2026 kabla ya kuanza kwa Mkutano Mkuu wa Nane wa GEF (GEF -8) uliowakutanisha karibu washiriki 2,000 kutoka serikalini, asasi za kiraia, taasisi za maendeleo na sekta binafsi.

Kwa Tanzania, ambayo ni miongoni mwa wanufaika wakubwa wa fedha za GEF Afrika Mashariki, mzunguko mpya wa ufadhili unafungua fursa zaidi za uwekezaji wa mazingira, ingawa changamoto ya upatikanaji wa fedha kwa ngazi za jamii bado ipo.

Fedha zilizoidhinishwa zinajumuisha dola 144.3 milioni kutoka mfuko mkuu wa GEF, dola 67.7 milioni kupitia Mfuko wa Nchi Masikini zaidi na Mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi (LDCF/SCCF), pamoja na dola milioni 20.5 kutoka Mfuko wa Kimataifa wa Bioanuwai (GBFF).

Akizungumza na waandishi wa habari, Kaimu Mtendaji Mkuu wa GEF, Claude Gascon, amesema kuidhinishwa fedha hizo ni ishara kuwa ushirikiano wa kimataifa bado una nafasi muhimu katika kufanikisha malengo ya mazingira duniani.

“Ahadi ya dola bilioni 3.9 inaonyesha dunia bado inaamini katika ushirikiano wa kimataifa ili kusaidia nchi zinazoendelea kufikia malengo ya mazingira ya mwaka 2030,” amesema.

Ameeleza mzunguko mpya wa ufadhili utajikita katika programu shirikishi za mazingira, ushirikishwaji mkubwa wa sekta binafsi na kuimarisha msaada kwa nchi zilizo hatarini pamoja na jamii za wenyeji. Takribani asilimia 35 ya rasilimali hizo zitaelekezwa kwa nchi maskini zaidi na mataifa madogo ya visiwani, huku asilimia 20 zikielekezwa kwa jamii za wenyeji na makundi ya wananchi wa ngazi za chini.

Hata hivyo, wadau wa mazingira kutoka Tanzania wanasema changamoto kubwa bado ni kuhakikisha fedha hizo zinawafikia walengwa wa vijijini.

Mratibu wa Kanda wa Mtandao wa Asasi za Kiraia wa GEF (GEF-CSO Network), Tumaini Marijani, amesema wananchi wengi, vikundi vya kijamii na mashirika madogo bado hawafahamu uwepo wa fursa za ufadhili kupitia programu kama GEF Small Grants Programme.

“Wengi hawajui kuwa fursa hizi zipo. Hata wanaozifahamu hukutana na masharti na taratibu za maombi ambazo ni ngumu kwa mashirika ya ngazi ya jamii,” amesema Marijani ambaye ni mwanaharakati wa mazingira kutoka Tanga, Tanzania.

Amependekeza matangazo ya ufadhili yatafsiriwe kwa Kiswahili na kusambazwa kupitia halmashauri, kata na taasisi za jamii ili kuongeza ushiriki wa wananchi. Pia ametaka Serikali kuimarisha mafunzo na uhamasishaji kwa vijana, wanawake na vikundi vya kijamii kuhusu namna ya kupata fedha za mazingira.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mikataba ya Mazingira na Mifuko ya GEF, Chizuru Aoki, amesema mwelekeo mpya wa GEF unasisitiza miradi inayounganisha masuala ya mabadiliko ya tabianchi, uhifadhi wa bioanuwai na maendeleo endelevu kwa wakati mmoja huku matokeo yake yakipimwa kwa uwazi.

Naye Mkuu wa Programu wa GEF, Dk Fred Boltz, amesema matumizi ya mfumo wa blended finance unaochanganya fedha za umma na sekta binafsi yatasaidia kuvutia uwekezaji mkubwa zaidi katika sekta ya mazingira.

“Fedha za umma ni muhimu kwa uhifadhi wa mazingira, lakini hazitoshi peke yake. Ushirikiano na sekta binafsi utasaidia kuongeza uwekezaji na kuharakisha ubunifu,” amesema.

Kwa mujibu wa GEF, kila dola moja inayowekezwa kupitia mfumo huo imefanikiwa kuvutia zaidi ya dola 18 za ziada kutoka vyanzo vingine vya fedha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *