Dar es Salaam. Katika jitihada za kuimarisha kipato kwa wafanyakazi wa serikali, Benki ya CRDB imetangaza kuongeza kiwango cha mtumishi kukopa sambamba na muda mrefu zaidi wa marejesho.

Mpango huo utakaodumu kwa miezi mitatu ya utekelezaji wa kampeni ya ‘Kopa Kimpango Wako’ inayotekelezwa na CRDB kuanzia sasa hadi mwishoni mwa Agosti mwaka huu, unawawezesha wafanyakazi wa Serikali kukopa bila dhamana yoyote kuanzia Sh100,000 hadi Sh300 milioni ambazo zitalipwa kwa kipindi cha hadi miaka 12.

Unafuu huo pia umetolewa kwenye mikopo ya nyumba ambayo mfanyakazi sasa anaweza kukopa hadi Sh3 bilioni kisha akalipa deni lake kwa kipindi hadi cha miaka 20.

Akitangaza maboresho hayo, Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi wa Benki ya CRDB, Stephen Adili amesema benki inatambua umuhimu wa kuwa na uchumi imara kuanzia ngazi ya mtu binafsi katika ustawi wa Taifa ndio sababu imekuja na huduma bunifu zinazomwezesha mteja kutimiza malengo yake ya kibiashara, uwekezaji na mengine ya kijamii.

“Kwa miongozo na ushirikiano mkubwa na Benki Kuu ya Tanzania ambayo ni mlezi wa sekta ya benki nchini, tumefanya mapitio ya viwango na muda wa marejesho kwa mikopo ya wafanyakazi wa Serikali.”

“Ninafurahi kuutangazia umma wa Watanzania kuwa sasa mtumishi anaruhusiwa kukopa kuanzia Sh100,000 hadi Sh300 milioni huku muda wa marejesho nao ukipanda kutoka miaka 10 mpaka 12 kwa riba nafuu ya asilimia 16 kwa mwaka ambayo huwezi kuipata mahali pengine popote,” amesema Adili.

Adili amesema kupungua kwa riba kumekusudia kumwongezea mfanyakazi wa serikali uwezo wa kukopa kiasi kikubwa zaidi kitakachomsaidia kukamilisha malengo yake yanayohitaji fedha.

Kutokana na umuhimu wa makazi bora ambayo Adili amesema ni msingi muhimu kwa ufanisi wa wafanyakazi katika kutekeleza majukumu yao, CRDB sasa inamruhusu mfanyakazi wa Serikali kukopa mpaka Sh3 bilioni ili kumpa fursa ya kujenga, kukarabati au kununua nyumba za ndoto zao.

“Jambo zuri kwa wafanyakazi wote wa Serikali ni kwamba, katika kipindi hiki pia tutakuwa tunanunua madeni waliyonayo katika taasisi nyingine za fedha. Nawakaribisha wafanyakazi wote wa Serikali kote nchini kuchangamkia fursa hizi za uwezeshaji tunazozitoa katika kampeni yetu ya ‘Kopa Kimpango Wako’,” amesisitiza Adili.

Kwa muda mrefu CRDB imekuwa kiungo muhimu katika kuchochea uchumi wa nchi kwa kutoa huduma bunifu za fedha ili kuwasaidia wafanyakazi kutimiza malengo binafsi na kujikwamua kiuchumi kwa makundi tofauti ya wafanyakazi wa Serikali.

Huduma hizi zinajumuisha akaunti ya mshahara ambayo licha ya kurahisisha kupokea mshahara kwa urahisi, inamuunganisha mfanyakazi na huduma za kidijitali kama SimBanking inayomwezesha kufanya miamala akiwa mahali popote.

Mteja mwenye akaunti ya mshahara pia anakuwa na bima inayotoa mkono wa pole wa Sh2 milioni endapo atafariki yeye mwenyewe au mwenza wake pamoja na kumruhusu kuomba mkopo binafsi wa kidijitali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *