
Wakazi walishambulia timu ya mazishi ya Ebola mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) katika jimbo la Kivu Kusini wiki hii, na kuwalazimisha wahudumu kuacha jeneza na kuzua hofu ya kuenea zaidi kwa maambukizi, wizara ya afya imesema.
Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa Ijumaa shambulio hilo lilitokea katika mji wa Katana, unaodhibitiwa na waasi wa AFC/M23 takribani kilomita 30 kaskazini mwa mji mkuu wa jimbo hilo, Bukavu.Hayo ni kwa mujibu wa wizara ya afya na mkuu wa hospitali ya eneo hilo aliyewaambia waandishi habari kuwa, “mashambulizi hayo yalilenga “timu ya mazishi salama na yenye heshima,” yaani wahudumu maalumu waliofunzwa kushughulikia miili yenye maambukizi makali kwa kufuata taratibu kali ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa.Baadaye mwili huo ulishughulikiwa na wanajamii, jambo ambalo ni hatari kubwa na linaweza kuchochea mlolongo mpya wa maambukizi.Wizara ya afya pamoja na afisa wa hospitali hawakubainisha sababu iliyochochea shambulio hilo.Tukio hilo linaonyesha kiwango cha kutokuaminiana na upinzani ambao bado unakwamisha juhudi za kudhibiti mlipuko huo, wakati mamlaka zikijaribu kuzuia kuenea kwa aina ya Bundibugyo ya virusi vya Ebola.Katika wiki za hivi karibuni, timu za mazishi na wahudumu wa afya wamekuwa wakilengwa katika mashambulizi, ikiwa ni pamoja na kutoka kwa baadhi ya ndugu wa marehemu wanaotilia shaka chanzo cha vifo hivyo.Katika tukio lingine kama hilo siku ya Jumatatu mjini Bunia, mji mkuu wa jimbo la Ituri ambako visa vya kwanza vya aina ya Bundibugyo vilithibitishwa, wakazi walishambulia timu ya wahudumu katika makaburi, na kusababisha angalau watu wanne kujeruhiwa, kwa mujibu wa ripoti hiyo na mfanyakazi wa misaada wa eneo hilo.Congo imerekodi visa 363 vilivyothibitishwa vya Ebola na vifo 62 tangu mlipuko wa hivi karibuni kutangazwa tarehe 15 Mei.