DAR ES SALAAM: SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), kwa kushirikiana na Shirika la Kazi Duniani (ILO) watazindua rasmi Kituo cha Msaada kwa Wafanyakazi Wahamiaji Tanzania (TUCTA-MWRC) chenye lengo la kusaidia watanzania wanaoenda kufanya kazi nje ya nchi.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Naibu Katibu Mkuu TUCTA Rehema Ludanga alisema kituo hicho kinachotarajiwa kufunguliwa Juni 11 mwaka huu jijini Dar es Salaam kupitia Mradi wa Better Regional Migration Management (BRMM) unaofadhiliwa na UK Foreign, Commonwealth and Development Office (UK-FCDO).

Amesema kuwa uzinduzi huo utafanyika katika jengo la WDC lililopo Barabara ya Lumumba, Dar es Salaam, ukiwa na lengo la kuimarisha uratibu wa masuala ya uhamaji wa wafanyakazi na kuhakikisha Watanzania wanaokwenda kufanya kazi nje ya nchi wanatumia njia salama na zinazotambuliwa kisheria.

Amesema kuwa TUCTA, kama msemaji na msimamizi mkuu wa haki na maslahi ya wafanyakazi nchini, imeanzisha kituo hicho ili kutoa taarifa sahihi, ushauri na mwongozo kwa wafanyakazi wanaokwenda kufanya kazi nje ya nchi pamoja na wageni wanaokuja kufanya kazi nchini Tanzania.

“Kituo hiki kitasaidia kuhakikisha haki, maslahi na ustawi wa wafanyakazi wahamiaji vinalindwa kupitia mikataba ya ajira iliyo wazi na inayozingatia maslahi yao,” amesema.

Mbali na huduma za ushauri, kituo hicho kitatoa mafunzo ya muda mfupi yatakayowasaidia wafanyakazi kujiandaa kwa mazingira ya kazi na maisha katika nchi wanazokwenda kufanya kazi, hatua inayolenga kuongeza uwezo wao wa kunufaika na fursa za ajira za kimataifa kwa usalama na ufanisi zaidi.

Aidha, wafanyakazi wa kigeni wanaokuja kufanya kazi nchini watapata fursa ya kujiunga na vyama vya wafanyakazi ili kuhakikisha haki na maslahi yao yanasimamiwa kikamilifu.

Kwa mujibu wa TUCTA, mpango huo pia unaunga mkono utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa kuchangia maendeleo ya rasilimali watu, kuongeza fursa za ajira na kuimarisha mchango wa Watanzania katika uchumi wa taifa.

Vilevile, umeelezwa kuwa mpango huo unaendana na juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, za kukuza diplomasia ya uchumi, kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na kufungua fursa zaidi za ajira na uwekezaji kwa Watanzania.

TUCTA na ILO wamewaalika wadau mbalimbali kutoka serikalini, sekta binafsi, vyama vya wafanyakazi, waajiri, taasisi za elimu na mafunzo, taasisi za fedha, mashirika ya kiraia, vyombo vya habari pamoja na washirika wa maendeleo kushiriki katika tukio hilo muhimu.

Wamesema ushiriki wa wadau utachangia mafanikio ya jitihada za kuhakikisha uhamaji na uhamiaji wa wafanyakazi unafanyika kwa usalama, uwazi na kwa kuzingatia haki na utu wa wafanyakazi wote ndani na nje ya Tanzania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *