
Vikosi vya ulinzi vya Iran jana usiku viliyatangwa kwa makombora maeneo kadhaa ya Israel, ikiwa ni katika kujibu mashambulizi yanayoendelea ya Israel dhidi ya Lebanon kwa kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano.
Sauti za ving’ora zilisika katika maeneo mengi ya Israel, ikiwa ni pamoja na Miinuko ya Golan, Tiberias, Safed, Nazareth, Haifa, na katika miji mingine kadhaa.
Jeshi la Israel limeeleza kuwa mifumo yake ya ulinzi wa anga bado iko katika hali ya tahadhari, huku wizara ya elimu ya utawala huo ikitangaza kufungwa kwa shule na vituo vyote vya elimu leo Jumatatu kutokana na hali ya usalama.
Iran imetekeleza oparesheni hii ikiwa ni jibu la moja kwa moja kufuatia kuendelea mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Lebanon, ikiwa ni pamoja na kitendo cha Israel cha kutumia mabomu ya fosforasi yaliyopigwa marufuku katika hujuma zake dhidi ya vitongoji vya kusini mwa Beirut (Dahiyeh).
Mara tu baada ya operesheni ya kulipiza kisasi, Makao Makuu ya Khatam al-Anbiya ambayo ni Kamandi Kuu ya Majeshi ya Iran, ilitahadharisha kuhusu “vipigo vikali zaidi na vya kujutia” iwapo mashambulizi ya Israel dhidi ya Lebanon yataendelea.
Katika taarifa yake, Kamandi Kuu ya Majeshi ya Iran imeukosoa utawala wa Kizayuni wa Israel kwa kukiuka kwa uratibu maalumu usitishaji vita na kushadidisha hujuma zake dhidi ya watu wa Lebanon kwa uungaji mkono wa moja kwa moja wa Marekani na kimya cha jamii ya kimataifa.