
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lleo Jumatano limefanya mjadala wa ngazi ya juu kuhusu kuendeleza suluhu za kisiasa Mashariki ya Kati huku migogoro, majanga ya kibinadamu na wasiwasi kuhusu uthabiti wa eneo hilo ukiendelea kuongezeka.
Wajumbe, mawaziri na maafisa wakuu wa Umoja wa Mataifa wamekusanyika katika Ukumbi wa Baraza la Usalama kwa kikao hicho, ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa taarifa kuhusu maendeleo ya hivi karibuni.
Guterres aonya Ukanda unaelekea katika janga kubwa zaidi
Akilihutubia Baraza hilo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, ameonya kuwa Mashariki ya Kati inakabiliwa na mgogoro unaozidi kuongezeka, wenye athari zinazovuka mipaka ya eneo hilo.
“Mashariki ya Kati inazidi kuvutwa katika mgogoro mkubwa zaidi, na matokeo yake yanafika mbali zaidi ya eneo hili,” amesema, akibainisha kuwa siku za karibuni zimeleta mashambulizi zaidi na kuzorota kwa hali ya usalama.
Ameeleza wasiwasi mkubwa kwamba maendeleo hayo yanaweza kusababisha kurejea kwa mapigano makubwa.
Lebanon yakabiliwa na kuongezeka kwa ghasia
Katibu Mkuu ameangazia hali inayozorota nchini Lebanon, ambapo mapigano yameongezeka tangu mwezi Machi.
Kwa mujibu wa Guterres, hali hiyo imesababisha vifo vya raia, watu zaidi ya milioni moja kulazimika kuhama makazi yao, uharibifu mkubwa kusini mwa Lebanon na vifo vya walinda amani saba wa Umoja wa Mataifa.
Amesisitiza umuhimu wa kufikia suluhisho la kidiplomasia na usitishaji mapigano wa kina, huku akikaribisha mazungumzo yanayoratibiwa na Marekani kati ya Israel na Lebanon.
Amewataka wahusika wote kuheshimu makubaliano yaliyopo, amesema “Hakuna mashambulizi tena. Hakuna visingizio tena.”
Usitishaji mapigano kati ya Marekani na Iran bado uko hatarini
Akizungumzia eneo la Ghuba, Guterres ameonya kuwa usitishaji mapigano kati ya Marekani na Iran bado ni dhaifu sana.
Ameuelezea kama “si usitishaji kamili wa mapigano bali ni kupungua kwa mapigano,” akionya dhidi ya kupuuzwa kwa hatari zilizopo.
Amesema “Hatupaswi kudharau uwezekano wa mapigano haya madogo kugeuka kuwa moto mkubwa zaidi, yaani vita kamili.”
Katibu Mkuu amebainisha kuwa vikwazo vya usafiri wa majini katika na karibu na Mlango Bahari wa Hormuz tayari vinaathiri masoko ya dunia kwa kuongeza bei za nishati na mbolea, kuvuruga minyororo ya usambazaji na kuongeza ukosefu wa chakula.
Amewataka wahusika wote kuheshimu usitishaji mapigano, kurejesha uhuru wa usafiri wa majini kwa mujibu wa sheria za kimataifa na kushiriki mazungumzo ya kina kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.
Pia ametambua juhudi za upatanishi zinazofanywa na mataifa ya eneo hilo, ikiwemo Pakistan.
UN yaongeza juhudi za kidiplomasia
Aliyeketi nyuma ya Katibu Mkuu wakati wa mjadala huo alikuwa Jean Arnault, mjumbe mkuu wa Umoja wa Mataifa anayesimamia juhudi za kidiplomasia kuhusu mgogoro huo.
Arnault hivi karibuni alitembelea Washington, ambako alikutana na maafisa wa Marekani na wataalamu wa sera kama sehemu ya mashauriano yanayoendelea ya kutafuta suluhisho endelevu la mgogoro huo.
Mazungumzo yake yalijikita katika juhudi za kidiplomasia za kikanda, ikiwemo mazungumzo yanayoratibiwa na Pakistan kati ya Marekani na Iran, pamoja na athari za kiuchumi zinazotokana na mgogoro huo.
Juhudi za amani zakumbwa na changamoto kubwa
Mkutano wa Baraza la Usalama unafanyika wakati ambapo hali ya uhasama kati ya Marekani na Iran imeongezeka tena.
Mazungumzo ya amani yako katika hatari kubwa kufuatia mashambulizi na mashambulizi ya kulipiza kisasi yaliyotokea usiku mmoja, ambayo ni ongezeko kubwa zaidi la mvutano tangu kufikiwa kwa usitishaji mapigano dhaifu mwanzoni mwa Aprili.
Mjadala huo unaongozwa na Rais wa Colombia, Gustavo Petro, na unatarajiwa kujikita katika mazungumzo, diplomasia na njia za kufikia amani ya kudumu katika eneo hilo.
FAO: tahadhari ya hali ya kibinadamu Gaza na Ukingo wa Magharibi
Kwa upande mwingine, Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limetoa taarifa kuhusu hali ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi, likionesha athari kubwa za mgogoro huo wa Mashariki ya Kati kwa uhakika wa chakula na maisha ya wananchi.
Shirika hilo limesema linahitaji dola milioni 72.5 mwaka huu ili kusaidia takriban kaya 30,500, lakini hadi sasa limepokea dola milioni 2.7 pekee.
Tathmini ya hivi karibuni imebaini kuwa mgogoro wa Gaza umesababisha uharibifu wa mfumo wa chakula wenye thamani ya dola bilioni 1.44 pamoja na hasara za kiuchumi zinazokadiriwa kufikia dola bilioni 1.46.
Msaada wafikia maelfu ya kaya za wafugaji
Licha ya upungufu wa fedha, FAO inaendelea kutoa msaada kwa familia zilizo katika mazingira magumu.
Zaidi ya kaya 5,000 zinazojishughulisha na ufugaji Gaza zimepokea shayiri bora na chakula cha mifugo, huku kaya 2,650 pia zikipatiwa vifaa vya huduma za mifugo ili kusaidia kuendeleza mifugo yao na maisha yao wakati mgogoro unaendelea.
Msisitizo wa diplomasia katika kipindi cha sintofahamu
Wakati vurugu, mateso ya kibinadamu na athari za kiuchumi zikiendelea kuongezeka Mashariki ya Kati, wanachama wa Baraza la Usalama wanatarajiwa kusisitiza umuhimu wa diplomasia, mazungumzo na suluhisho za kisiasa ili kuzuia eneo hilo kutumbukia katika mzozo mkubwa zaidi.