
Katibu Mkuu Guterres pia amelaani kuendelea kushikiliwa kwa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa waliokamatwa katika miaka ya 2021, 2023 na 2025, akitaka waachiliwe mara moja na bila masharti yoyote.
Kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo na Naibu Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Farhan Haq, imeelezwa kuwa hadi sasa wafanyakazi 73 wa UN bado wanazuiliwa kiholela, huku mfanyakazi mmoja wa Umoja wa Mataifa akifariki akiwa kizuizini.
Aidha, taarifa hiyo imesema baadhi ya wafanyakazi hao wanashikiliwa bila kuruhusiwa kuwasiliana na familia zao au kupata huduma za kisheria, hali ambayo inakiuka sheria za kimataifa, inasababisha mateso makubwa kwa familia zao na kuathiri uwezo wa Umoja wa Mataifa na washirika wake kuwafikishia misaada mamilioni ya watu wenye uhitaji nchini Yemen.
Umoja wa Mataifa umesisitiza kuwa wafanyakazi wake, wakiwemo raia wa Yemen wanaofanya kazi kwa niaba ya shirika hilo, wanastahili kinga dhidi ya hatua za kisheria kwa kazi wanazozifanya katika majukumu yao rasmi.
Katibu Mkuu ameeleza umuhimu wa kuendelea kwa mazungumzo na mawasiliano na mamlaka za Wahouthi ili kuhakikisha wafanyakazi hao wanaachiliwa na shughuli za kibinadamu na maendeleo zinaweza kuendelea tena.
Amesema “Umoja wa Mataifa utaendelea kutumia njia zote zinazowezekana kuhakikisha wafungwa hao wanaachiwa huru kwa usalama,” huku akieleza mshikamano wake kamili kwao na familia zao.
Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa pia amesisitiza kuwa wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu hawapaswi kulengwa kwa kuzuiliwa kutokana na kazi yao muhimu ya kuokoa na kuboresha maisha ya watu.
Amehitimisha kwa kusisitiza kuwa Umoja wa Mataifa utaendelea kuwa bega kwa bega na wananchi wa Yemen katika kutimiza azma yao ya kupata amani ya haki na ya kudumu.