WASTANI wa pato la taifa kwa mtu mmoja mmoja nchini umeongezeka kwa asilimia 7.4 na kufikia shilingi 3,544,124 sawa na dola za Marekani 1,390 mwaka 2025, ikilinganishwa na shilingi 3,299,637 sawa na dola 1,264 mwaka 2024.

‎Akizungumza bungeni mjini Dodoma wakati akiwasilisha Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2025 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/27, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, amesema ongezeko hilo limetokana na ukuaji mzuri wa uchumi wa taifa katika kipindi husika.

‎Profesa Mkumbo amesema kuwa kwa mujibu wa takwimu mpya za mwaka wa kizio wa 2019, pato halisi la taifa lilikua kwa wastani wa asilimia 5.9 mwaka 2025 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 5.6 mwaka 2024. ‎Amefafanua kuwa kwa bei za mwaka 2019, pato la taifa lilifikia shilingi trilioni 234.104 mwaka 2025, sawa na dola za Marekani bilioni 91.81, kutoka shilingi trilioni 211.975, sawa na dola bilioni 81.2 mwaka 2024.

‎Waziri huyo amesema matokeo hayo yanaashiria kuendelea kuimarika kwa uchumi wa nchi na kuongeza uwezo wa wananchi kushiriki katika shughuli za uzalishaji na maendeleo ya kijamii na kiuchumi.SOMA: Ukuaji Pato la Taifa kufikia asilimia 6.9

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *