
Wakati ambapo macho yote yameelekezwa kwenye viwanja vya mashindano ya Kombe la Dunia huko Marekani, Mexico na Canada, Mswizi Joseph Blatter, rais wa zamani wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), ameelekeza mishale ya hasira yake kwa mrithi wake Gianni Infantino na nchi mwenyeji mwenza Marekani, akiimbusha dunia kuwa “shujaa wa FIFA” anafuatilia mashindano hayo kwa uchungu.
Katika taarifa nzito kwa gazeti la Ufaransa la L’Equipe, Blatter mwenye umri wa miaka 90 ametumia fursa ya mgogoro wa kuzuiwa mwamuzi wa Somalia, Omar Artan kuingia katika ardhi ya Marekani kushambulia vikali uongozi wa Giovanni Infantino, akitaja kilichotokea kuwa ni cha “kipuuzi na aibu.”
Blatter anasema tukio la kuzuiwa mwamuzi wa Kisomali, Omar Artan, kuingia Marekani halikuwa kosa la kiutawala au utaratibu wa usalama tu, bali ni “dhambi kubwa” inayogusa kiini cha kujitegemea mpira wa miguu, ikizingatiwa kwamba kufanyika mashindano ya Kombe la Dunia katika nchi inayomzuia mwamuzi aliyeidhinishwa na FIFA kuingia katika ardhi yake ni ukiukaji wa kanuni za mchezo huo.
Mashambulizi ya Blatter yamekuwa na sura mbili za kiufundi na kisiasa akimtaka Infantino kuthibitisha kwamba “ana nguvu kuliko rafiki yake wa karibu katika Ikulu ya White House.”
Joseph Blatter amedokeza kwamba Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), amekuwa “mateka” kwa matakwa ya siasa za Marekani na sheria kali za uhamiaji, badala ya kuwa bwana wa maamuzi yake mwenyewe.
Omar Artan, ambaye ni miongoni mwa waamuzi bora wa Afrika na yumo katika orodha ya waamuzi 52 wa Kombe la Dunia ya FIFA, amezuiliwa na serikali ya Marekani kuingia nchini humo na kurejeshwa Somalia kutokana na kile kilichoitwa “masuala ya uhakiki wa kiusalama”.
Rais Trump wa Marekani amekuwa akitoa matamshi ya kibaguzi na chuki dhidi ya Somalia na Wasomali na hiyo imetajwa kuwa sababu kuu ya kuzuiwa refa hiyo maarufu barani Afrika kuingia Marekani.
Itakumbukwa pia kwamba, zaidi ya robo ya nchi zinazoshiriki katika Kombe la Dunia, nyingi zikiwa ni za Afrika, zinaathiriwa na vizuizi vya kusafiri na zinakabiliwa na viwango vya juu vya kukataliwa visa za maafisa na mashabiki wao.
Mashindano hayo yalianza jana Alkhamisi nchini huko Mexico City, ambapo Afrika Kusini imekutana na wenyeji wenza, Mexico, katika mechi ya ufunguzi ambapo Afrika Kusini imetandikwa mabao mawili kwa nunge. Katika mchezo huo, imeshuhudiwa kadi nyekundu tatu zikionyeshwa ambapo mbili zimeenda upande wa Afrika Kusini na moja ikienda Mexico.