SINGIDA Black Stars inaweza kuingia sokoni kutafuta mbadala wa kiungo wake tegemeo, Morice Chukwu, baada ya nyota huyo kuweka wazi kuwa yupo mbioni kuondoka kwenye kikosi hicho mwishoni mwa msimu huu.

Kiungo huyo raia wa Nigeria amefichua kuwa tayari ameanza mchakato wa kuondoka Singida Black Stars, huku akieleza kuwa wakala wake anatarajiwa kuwasiliana na uongozi wa klabu hiyo kuujulisha rasmi uamuzi wake.

Kauli ya Chukwu imeibua maswali mengi ndani ya kambi ya Singida Black Stars kutokana na mchango mkubwa alioutoa tangu alipotua kikosini hapo, huku baadhi ya mabosi wakihofia kuwa kuondoka kwake kunaweza kuacha pengo kubwa katikati ya uwanja.

Katika mazungumzo yake na Mwanaspoti kwa njia ya simu, Chukwu alifafanua msimamo wake kuhusu hatma yake ndani ya klabu hiyo, huku akiweka wazi kwamba bado hajajua hatma yake msimu ujao.

“Kulikuwa na kikao kati ya Singida na wakala wangu lakini pande zote mbili zimefikia makubaliano kwamba msimu unaofuata sitakuwepo ndani ya kikosi cha Singida,” alisema Chukwu.

Alipobanwa zaidi kuhusu atakakoelekea baada ya kuondoka Singida, kiungo huyo alijibu kwa kifupi akisema: “Sina timu kwa sasa,”akimaanisha bado hajafikia makubaliano na klabu yoyote kuelekea msimu ujao.

Rekodi zinaonyesha Chukwu alitua Singida mwaka 2023 akitokea Rivers United ya Nigeria kwa mkataba wa miaka mitatu. Tangu wakati huo amekuwa mmoja wa wachezaji waliobadilisha sura ya kikosi hicho kutokana na uwezo wake wa kucheza nafasi zaidi ya moja.

Mbali na kucheza kama kiungo mkabaji, nyota huyo amekuwa akitumika pia kama kiungo wa kati na wakati mwingine beki wa kati pale timu inapohitaji, jambo lililomfanya kuwa mmoja wa wachezaji wanaoaminika zaidi na benchi la ufundi.

Katika misimu miwili aliyokuwa Singida Black Stars, Chukwu ameshiriki safari ya timu hiyo katika mashindano mbalimbali ya ndani na nje ya nchi, akichangia kwa kiasi kikubwa uimara wa kikosi hicho kilichojitengenezea ushindani dhidi ya vigogo wa Ligi Kuu Bara.

Singida imebakiza mechi tano dhidi JKT Tanzania, Juni 13, 2026, Dodoma Jiji Juni 24,Tanzania Prisons Juni 27,Simba Juni 27 na Fountain Gate, Juni 30.

Iwapo itashinda mechi zake zote itajihakikishia kumaliza nafasi ya nne na kuwa katika nafasi nzuri ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *