
NYOTA wa Simba, Libasse Gueye, ameshindwa kujizuia kwa kiungo mkongwe wa timu hiyo, Clatous Chama, akimtaja kama mchezaji mwenye akili kubwa zaidi ya mpira kati ya wale aliowahi kucheza nao kwenye timu moja.
Gueye ambaye ni raia wa Senegal alisema Chama sio mchezaji wa kawaida, bali ni ‘ubongo wa mchezo’ ambaye huamua kasi, mwelekeo na hatima ya mashambulizi bila kuonekana akifanya kazi kubwa.
Wachezaji wote hao waliingia kwenye timu hiyo katika dirisha dogo la usajili na wamekuwa na kiwango bora zaidi kwenye timu hiyo ambayo kwa sasa inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi.
Akizungumzia kiwango cha staa huyo raia wa Zambia, Libase alisema ni mchezaji mkubwa ambaye amekuwa akionyesha kiwango kilekile kwenye kila mchezo ambao amekuwa akipata nafasi uwanjani.
“Chama anaona mpira kabla haujafika. Wakati mwingine unakimbia, hujapata hata pasi lakini tayari yeye ameshauweka mpira pale unapotakiwa kuwa,” alisema Gueye.
Tangu arejee Simba, Chama ameendelea kuonyesha tofauti kubwa ya kiufundi, akibeba jukumu la kuunganisha kiungo na safu ya ushambuliaji kiasi cha kuweka rekodi ya kushinda tuzo ya mchezaji bora wa mechi mara tano mfululizo katika mechi za Ligi Kuu Bara.
Kwa sasa Chama ndiye kinara wa mabao kwa Simba akiwa amefumania nyavu mara nane huku akiwa na asisti nne sawa na Seleman Mwalimu mwenye asisti moja, akifuatiwa na Gueye mwenye mabao sita.
Uzoefu wake wa kucheza soka la kulipwa Tanzania kwa miaka minane sasa, umempa nafasi ya kuelewa ligi, kitu kinachomfanya kuendelea kutesa.
Gueye aliongeza kwa kusema; “Unapocheza na Chama unajiona mwepesi. Anakufanya uelewe mpira kwa njia tofauti. Sio nguvu tu, ni akili pia.”
Kwa mujibu wa benchi la ufundi la Simba, Chama ambaye kwa sasa anauguza majeraha ni mchezaji anayetoa suluhisho hata pale timu inapokuwa nyuma, kutokana na ubunifu wake.
Uhusiano wa Chama, Gueye, Anicet Oura na Ellie Mpanzu umeongeza nguvu kwenye kikosi hicho huku wakionekana kuelewana kwa haraka katika mashambulizi ya pasi fupi na kwa mashambulizi ya kustukiza.