Dodoma. Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limetoa siku nne kwa vijana waliomaliza kidato cha sita ambao hawajaripoti jeshini, waende katika kambi zilizopo karibu na maeneo yao.

Vijana hao wanatakiwa kuripoti katika kambi zote nchini isipokuwa kambi za Ruvu, Makutupora na Chuo cha Uongozi cha JKT (CUJKT) kilichopo Kimbiji.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya JKT Chamwino leo Juni 12, 2026, Mkuu wa Tawi la Operesheni na Mafunzo JKT, Brigedia Jenerali Peter Mnyani, amesema vijana hao wamepewa fursa nyingine ili wakajiunge na mafunzo hayo.

Amesema siku zimeongezwa kuanzia leo Juni 12, 2026 hadi Juni 15, 2026 na kwamba vijana ambao walishindwa kujiunga kutokana na changamoto mbalimbali ni muhimu wakatumia fursa hiyo.

“Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa, Meja Jenerali Rajabu Mabele, ametoa nafasi kwa vijana ambao walikuwa na changamoto mbalimbali za kifamilia, kuripoti kwenye kambi zilizo karibu kuanzia leo hadi Juni 15. Tunaomba watumie fursa hiyo bila kukosa,” amesema Brigedia Jenerali Peter Mnyani.

Awali JKT ilitangaza nafasi 60,000 kwa vijana waliomaliza kidato cha sita mwaka 2026 ambapo walitakiwa kujiunga katika mafunzo hayo kwa mujibu wa sheria kuanzia Juni Mosi, 2026 na mwisho ulikuwa Juni 7, 2026.

Hata hivyo, taarifa zinaonyesha tangu mwanzo JKT ilikuwa ikiwapokea vijana kwenye kambi zote hata kama walikuwa wamepangiwa kambi nyingine, na kwa sasa wanaendelea na mafunzo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *