Kigoma. Ukarabati wa Meli kongwe katika Ziwa Tanganyika ya MV Liemba iliyokuwa ikifanya safari zake katika nchi za Tanzania, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Zambia, umefikia asilimia 75 huku ikitarajiwa kuanza kutoa huduma ifikapo Agosti 2026.

Ukarabati wa Meli ya hiyo yenye uwezo wa kubeba abiria 600 na tani 200 za mizigo unafanywa na Mkandarasi M/S Brodosplit JSC ya nchini Croatia kwa kushirikiana na Dar es Salaam Merchant Group (DMG) ya nchini Tanzania ambapo kukamilika kwake itaongeza fursa za usafirishaji na biashara katika ukanda wa Ziwa Tanganyika.

Akizungumza na waandishi wa Habari Juni 11, 2026 wakati wa ukaguzi wa mradi huo, Katibu tawala Mkoa wa Kigoma, Hassan Rugwa amesema majaribio ya awali ya MV Liemba yanatarajiwa kuanza Julai kabla ya kuanza rasmi kutoa huduma Agosti.

“Kazi zilizobakia ni kufanya majaribio ya meli hii watalamu wametuhakikishia kwamba mwezi wa saba tuanze kufanya majaribio na mwezi wa nane ianze kutoa huduma.

Meli kongwe ya MV Liemba inayoendelea kufanyiwa matengenezo na ukarabati mkoani Kigoma, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha usafiri wa majini katika Ziwa Tanganyika.

“Kukamilika kwa ukarabati huu unatoa nafasi ya kukarabati kwa meli nyingine ya MV Mwongozo ni meli yetu ya pili ya kihistoria ukiachana na hii.”

Pia, Rugwa amefanya ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa miradi ya maboresho ya Bandari ya Kigoma katika Ziwa Tanganyika ambapo inaendelea  inatarajiwa kuongeza ufanisi wa huduma za usafiri wa majini na biashara ndani na nje ya nchi.

Mradi huo wenye thamani ya Dola za marekani 20 milioni, ukihusisha kuongeza kina cha bandari na ujenzi wa gati lenye urefu wa mita 150 kwa ajili ya kuegesha meli za abiria ambapo utakapokamilika Oktoba 2027 utawezesha meli mbili kutoa nanga kwa wakati mmoja.

“Kimsingi hapa tunazo terminal mbili ya abiria, lakini pia terminal ya mizigo na zote zipo kwenye miradi ya ukarabati kwa kufanya upanuzi pamoja na ujenzi, amesema Rugwa.”

Amesema miradi hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha usafiri wa majini nchini.

Rugwa amewakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara kutumia fursa zitakazotokana na maboresho hayo, huku akibainisha kuwa ukamilishaji wa MV Liemba utafungua njia ya kuanza kwa ukarabati wa meli nyingine ya kihistoria ya MV Mwongozo.

Naye Humphrey Mwambungu kutoka Kampuni ya Meli Tanzania (Tashico), amesema uwekezaji wa Serikali katika ukarabati wa meli ya Mv Liemba utawanufaisha kiuchumi wananchi na wafanyabiashara wa ngazi zote kuanzia wajasiriamali hadi wafanyabishara wakubwa.

Aidha, Mwambungu amesema kuwa kwa sasa hakuna meli yenye uwezo wa kubeba watu na mizigo inayofanya kazi katika ziwa Tanganyika.

“Vitu ambavyo vilikuwa vinasubiliwa vimeshafika kulikuwa na shaft na propeller zimeshafika, kazi zilizobaki kwa sasa tunasema fitting tunatarajia mwishoni mwa mwezi wa saba mradi huo kuwa umekamilika, amesema.”

Ukarabati huo ulianza Julai 13, 2024 na ulitarajiwa kukamilika baada ya mwaka mmoja na nusu, hata hivyo ulichelewa baada ya kukawia kuwasili kwa mahitaji katika hatua za awali, maji ya ziwa kujaa na kusababisha meli kushindwa kupanda kwenye chelezo ili kuweza kutoa ‘shaft na propeller.’

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *