
Dar es Salaam. Shirika la Reli Tanzania (TRC) limeongeza safari ya treni ya umeme (SGR) kati ya Dodoma na Dar es Salaam huku likitangaza kurejea rasmi kwa huduma za usafiri wa abiria kwa kutumia treni za reli ya zamani ya MGR kuelekea mikoa ya Kigoma, Mwanza, Moshi na Arusha, hatua inayolenga kukidhi ongezeko la mahitaji ya usafiri nchini.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa leo, Juni 12, 2026, na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma cha TRC, Fredy Mwanjala, treni ya ziada ya EMU itaondoka Dodoma kuelekea Dar es Salaam saa 1:00 usiku wa leo, Ijumaa, Juni 12, 2026.
Uamuzi huo umetokana na kuongezeka kwa idadi ya wasafiri wanaotumia huduma ya reli ya kisasa ya SGR, huku shirika hilo likiahidi kuendelea kutoa huduma bora, salama na za uhakika kwa wananchi.
“TRC inawashauri wasafiri kukata tiketi mapema kupitia mfumo rasmi wa ukataji tiketi uliopo kwenye stesheni na kwenye mtandao ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza,” imeeleza taarifa hiyo.
Katika hatua nyingine, shirika hilo limetangaza kurejea kwa huduma za treni za MGR ambazo zilikuwa zimesitishwa tangu Desemba 2025 baada ya daraja la Kidete kusombwa na maji kutokana na mvua.
Kwa ratiba mpya, safari za kwenda Kigoma, Mwanza, Moshi na Arusha zitaanza rasmi Juni 18, 2026.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa treni ya Deluxe itaondoka Dar es Salaam kwenda Mwanza kila Alhamisi saa 2:00 asubuhi, huku safari za kuelekea Arusha kupitia Moshi zikifanyika kila Ijumaa saa 8:30 mchana.
Aidha, treni ya Ordinary kuelekea Kigoma itaondoka Dar es Salaam kila Jumapili saa 9:30 alasiri.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, huduma hizo zitafanyika mara mbili kwa wiki kwa baadhi ya mikoa ili kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata usafiri wa uhakika wakati wa kipindi hiki cha ongezeko la mahitaji ya usafiri.