Hayo yamebainishwa katika ripoti mpya ya UNAIDS iliyotolewa leo ambayo inaonesha kuwa misaada ya maendeleo duniani ilipungua kwa asilimia 23 mwaka 2025, kikwa ni kiwango kikubwa zaidi kuwahi kurekodiwa, na kuathiri vibaya programu za VVU katika nchi maskini zenye mzigo mkubwa wa maambukizi.

© WHO/Asad Zaidi Mtaalamu wa maabara anafanya kipimo cha uchunguzi wa VVU katika kituo cha matibabu huko Hayatabad katika wilaya ya Peshawar nchini Pakistan.

Akizungumzia ripoti hiyo kutoka Geneva uswisi Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS, Winnie Byanyima amesema “Hakuna shaka kuwa huu ndio mtikisiko mkubwa zaidi katika mwitikio wa VVU tangu dunia ilipoamua kupambana na ugonjwa hu.” 

Katika kipindi cha mwaka 2024 hadi 2025, huduma za upimaji wa VVU zilishuka kwa asilimia 22, huku matumizi ya dawa za kujikinga na maambukizi ya VVU (PrEP) yakipungua kwa asilimia 38 katika nchi 62 zilizowasilisha taarifa kwa UNAIDS.

Aidha, ufadhili wa kondomu umepungua kwa zaidi ya asilimia 90 katika baadhi ya maeneo.

Mafanikio yaliyopatikana yako hatarini

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, vifo vinavyotokana na UKIMWI vimepungua kwa asilimia 56 tangu mwaka 2010, huku maambukizi mapya yakishuka kwa asilimia 43. Hivi sasa watu milioni 32.1 kati ya milioni 40.9 wanaoishi na VVU wanapata matibabu.

Hata hivyo, karibu watu milioni 9 bado hawapati tiba, hali inayoongeza hatari ya kuongezeka kwa vifo na maambukizi mapya, hasa katika maeneo yanayotegemea ufadhili wa nje.

Ripoti hiyo pia inaonesha kuwa kila wiki wasichana 3,000 Barani Afrika Kusini, mwa Jangwa la Sahara wanaambukizwa VVU.

UNAIDS Nigeria Grace Amodu, alitambua kuwa ana VVU alipokuwa na umri wa miaka 7. Sasa ana watoto wawili na wote hawana maambukizi ya VVU kutokana na huduma za kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, PMTCT.

Kubanwa kwa haki za binadamu kunaongeza hatari

UNAIDS imeonya kuwa kuongezeka kwa sheria zinazoyabagua makundi yaliyo pembezoni kunawafanya watu wengi kuogopa kupima VVU au kutafuta matibabu.

“Magonjwa huenea kwa kasi zaidi pale ambapo haki za binadamu zinalindwa kwa kiwango cha chini. Kuporomoka kwa haki za binadamu na nafasi ya kiraia kuna athari kubwa kwa afya ya umma na mapambano dhidi ya VVU,” amesema Byanyima.

Wito wa kuimarisha uwekezaji

Ripoti hiyo inaeleza kuwa bado inawezekana kutokomeza UKIMWI kama tishio la afya ya umma ifikapo mwaka 2030 ikiwa nchi zitaongeza uwekezaji wa ndani na washirika wa maendeleo wataendelea kuunga mkono juhudi hizo.

UNAIDS imeonya kuwa kushindwa kuchukua hatua sasa kunaweza kufuta mafanikio ya miongo kadhaa ya mapambano dhidi ya UKIMWI.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *