Kamanda wa Makao Makuu ya Majeshi ya Iran, Khatamul-Anbiya (SAW) ameionya Marekani kuhusu “mzunguko wa uongo, tasa na wenye migongano” katika mienendo yake, baada ya Washington kutishia kwanza kwamba itashambulia miundombinu ya nishati ya Iran na kisha kudai mazungumzo yameidhinishwa.

“Marekani, kwa upande mmoja, inazungumzia makubaliano na mazungumzo, na kwa upande mwingine inafanya uovu,” amesema Meja Jenerali Ali Abdollahi katika taarifa yake iliyotolewa Alhamisi.

Onyo lake limekuja baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kutishia kwanza “kuipiga VIKALI SANA Iran USIKU WA LEO” na kuteka Kisiwa cha Kharg, kisha saa kadhaa baadaye akatangaza “amefuta mashambulizi yaliyopangwa dhidi ya Iran,” akidai mazungumzo “yamefika katika ngazi ya juu ya uongozi wa Iran na kuidhinishwa.”

“Mgongano huu wa wazi katika mienendo na matamshi ya Marekani ndio chanzo kikuu cha ukosefu wa usalama katika eneo la Magharibi mwa Asia na umehatarisha usalama wa biashara na uchumi wa kimataifa, hasa Lango-Bahari la Hormuz,” Jenerali Abdollahi amesema.

Abdollahi amesema viongozi wa Marekani, kutokana na “ukosefu wa uelewa sahihi kuhusu taifa la Iran lenye heshima na ujasiri na vikosi vya jeshi lake lenye nguvu, wanafuatilia mzunguko wa uongo na tasa” wa Marekani.

Kamanda huyo ameonya kwamba kama Marekani itafanya mashambulizi zaidi dhidi ya Iran, “moto wa vita utapanuka na kuwa mkubwa zaidi, na kueneza ukosefu wa usalama katika kanda nzima”.

Meja Jenerali Ali Abdollahi amesisitiza kwamba Vikosi vya Jeshi la Iran vitaendelea kuwa katika hali ya “utayarifu kamili, umakini na udhibiti wa kipelelezi” na “vitajibu kwa dhati tishio lolote dhidi ya usalama, mamlaka, na ardhi ya nchi kwa operesheni athirifu, chungu na zitakazosababisha majuto”.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *