
Kamanda wa Makao Makuu ya Majeshi ya Iran, Khatamul-Anbiya (SAW) amesema kuwa hivi karibuni ulimwengu utasikia mwangwi wa ushindi wa Iran, na ushindi wa muqawama dhidi ya adui mchokozi na gaidi.
Meja Jenerali Ali Abdollahi ameyasema hayo katika ujumbe wake katika marasimu ya kutimia mwaka mmoja tangu kuuawa shahidi Meja Jenerali Gholamali Rashid na mwanawe Amin Abbas Rashid yaliyofanyika Ijumaa jioni huko Dezful.
Sayyid Ali Khamenei Kiongozi wa Mapinduzi alimteuwa Jenerali Rashid mwaka 2016 kuwa Kamanda wa Khatamul-Anbiya. Ayatullah Khamenei aliuawa shahidi katika mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran Februari 28 mwaka huu. Jenerali Rashid alikuwa akihudumu katika nafasi hiyo hadi alipouawa shahidi.
Jenerali huyo wa ngazi ya juu wa Iran na mwanawe waliuawa shahidi katika hujuma ya kichokozi ya Israel dhidi ya Iran Juni 13, 2025.
Katika ujumbe wake, Meja Jenerali Abdollahi ameeeleza kuwa, ingawa kuuawa shahidi Jenerali Rashid ilikuwa pigo kubwa, lakini kwa mara nyingine tena Iran ya Kiislamu iliudhihirishia ulimwengu uwezo wake wa kuilinda na kuihami nchi.
“Adui dhaifu na katili alidhani kwamba kwa kutekeleza mauaji ya kigaidi dhidi ya viongozi wakuu wa kijeshi wa Iran angeweza kuvunja irada na azma thabiti ya Iran ya kuilinda nchi. Adui hakujua kwamba Rashid aliyeuawa shahidi ameacha nyuma urithi wa maarifa, tajiriba na fikra za kimkakati za kuongoza vizazi vijavyo vya nchi hii,” ameeleza Meja Jenerali Ali Abdollahi Kamanda wa Makao Makuu ya Majeshi ya Iran, Khatamul-Anbiya (SAW).