
Ofisi inayohusika na kuhifadhi na kuchapisha kazi za Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu imetangaza ratiba ya hafla za kuaga, mazishi, na kuzikwa kwa Shahidi Ayatullah Imam Sayyid Ali Khamenei.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ofisi hiyo, hafla za kuaga mwili wa Kiongozi Shahidi zitafanyika katika Msala wa Imam Khomeini mjini Tehran tarehe 4 na 5 Julai, zinazolingana na tarehe 19 na 20 za mwezi wa Muharram.
Msafara wa mazishi mjini Tehran umepangwa kufanyika tarehe 6 Julai, huku msafara mwingine wa mazishi ukitarajiwa kufanyika katika mji mtukufu wa Qom tarehe 7 Julai.
Hafla ya mwisho ya mazishi itafanyika katika mji mtukufu wa Mashhad tarehe 9 Julai, sambamba na mkesha wa kumbukumbu ya shahada ya Imam Sajjad (AS). Taarifa hiyo imeeleza kuwa Kiongozi Shahidi atazikwa katika Haram tukufu ya Imam Ridha (AS).
Waandalizi wamewaalika “watu wote watukufu na wapendwa, watu huru wa dunia, wafuasi wa madrasah ya Uislamu, na wote wanaoipenda Iran” kushiriki katika hafla hizo na kutoa heshima za mwisho kwa Kiongozi Shahidi.
Taarifa hiyo pia imezishukuru taasisi za serikali na makundi ya wananchi kwa maandalizi makubwa yaliyofanywa, ikisisitiza kuwa jukumu kuu katika kuandaa hafla hizo litakuwa mikononi mwa wananchi wenyewe kama “wamiliki halisi wa maombolezo,” na kuongeza kuwa ushiriki wa watu kwa kiwango kisicho na mfano unatarajiwa.
Maelezo zaidi kuhusu hafla hizo yatatangazwa baadaye.
Ayatullah Khamenei aliuawa shahidi na majeshi ya kigaidi ya Marekani na Israel katika makazi yake mjini Tehran tarehe 28 Februari, wakati tawala hizo mbili zilipoanzisha vita vya uchokozi dhidi ya Iran ambavyo pia vilishuhudia kuuawa kwa makamanda kadhaa wa juu wa kijeshi.
Siku chache baadaye, Baraza la Wataalamu la Iran, chombo chenye wanazuoni 88 wa Kiislamu, lilimchagua Ayatullah Sayyid Mojtaba Khamenei mwenye umri wa miaka 56 kuwa Kiongozi wa tatu wa Mapinduzi ya Kiislamu. Ayatullah Sayyid Mojtaba Khamenei ni mwana wa Shahidi Ayatullah Sayyid Ali Khamenei.