Maafisa wakuu wa Iran wameadhimisha mwaka mmoja tangu kuanza kwa Vita vya Siku 12, vilivyoanza tarehe 13 Juni mwaka uliopita kufuatia mashambulizi ya kichokozi ya anga ya utawala haramu wa Israel, na ambayo yaliua makamanda kadhaa wa juu wa kijeshi, maafisa wa serikali, pamoja na wanasayansi wa nyuklia.

Mkuu wa Idara ya Mahakama ya Iran, Gholam Hossein Mohseni‑Ejei, aliandika katika mitandao ya kijamii siku ya Jumamosi kwamba “umoja wa kitaifa wa kushangaza” ndani ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran umeuacha ulimwengu “ukishangaa na kukanganyikiwa.”

Amesema: “Ushikamano huu thabiti na umoja umeiletea nchi yetu nguvu ya ziada ya kuzuia vitisho.” Ameongeza kuwa: “Wote wajue kwamba. hatuna kabisa imani na Wamarekani. Kutokuamini huku kunatokana na ukweli na matukio ya kihistoria,” amesema, akiashiria mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja na Marekani.

Mohseni‑Ejei amebainisha kuwa wakati wa Vita vya Siku 12, sehemu zote za Vikosi vya Ulinzi vya Iran zilionyesha uwezo mkubwa chini ya uongozi wa Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei.

Tarehe 13 Juni, Israel ilianzisha vita vya uchokozi dhidi ya Iran kwa kuwaua kwa kulenga moja kwa moja maafisa wa juu wa Iran, wakiwemo makamanda wa kijeshi na wanasayansi wa nyuklia, pamoja na raia.

Zaidi ya wiki moja baadaye, Marekani pia iliingia katika vita hivyo kwa kushambulia kwa mabomu vituo vitatu vya nyuklia vya Iran, hatua iliyokiuka kwa kiwango kikubwa Mkataba wa Umoja wa Mataifa, sheria za kimataifa, na Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia (NPT).

Kujibu mashambulizi hayo, Vikosi vya Ulinzi vya Iran vililenga maeneo ya kimkakati katika ardhi zinazokaliwa na Israel, pamoja na kambi ya anga ya al‑Udeid nchini Qatar, ambayo ni kituo kikubwa zaidi cha kijeshi cha Marekani katika eneo la Asia Magharibi. Marekani na Israel zililazimika kuomba usitishaji vita kufuatia operesheni hizo kali za ulipizaji kisasi za Iran.

Kwa upande Ayatullah Sadegh Amoli Larijani, mkuu wa Baraza la Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu Iran, pia ameandika katika mitandao ya kijamii kuwakumbuka majenerali mashuhuri waliouawa katika Vita vya Siku 12.

Amesema: “Mwaka mmoja baadaye, imekuwa wazi zaidi kuliko wakati mwingine wowote kwamba maadui wa Iran, pamoja na uovu na uhalifu wao wote, hawakufanikiwa kufikia malengo yao maovu.”

Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Baqer Qalibaf, naye ameadhimisha kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu kuanza kwa vita hivyo katika ujumbe aliouchapisha kwenye akaunti yake binafsi ya X siku ya Jumamosi.

Amesema: “Mwaka mmoja umepita tangu duru ya kwanza ya mashambulizi ya kihalifu ya utawala wa Israel na Marekani dhidi ya nyumba yetu ya milele, Iran. Waliwaua watoto wasio na hatia na hawakusita kufanya uhalifu au ukatili wowote.”

Wakati huo huo, Ubalozi wa Iran mjini Berlin umetoa taarifa ukisema kwamba “yaliyotokea katika siku zile hayakuwa tu shambulio dhidi ya Iran, bali yalikuwa shambulio la wazi dhidi ya diplomasia, ukiukaji wa wazi wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa, na kupuuzwa kwa misingi ya kimsingi ya sheria za kimataifa.”

Taarifa hiyo iliendelea kubainisha kwamba jambo lisilosahaulika ni “ukimya wa wale waliofumba macho kwa makusudi” mbele ya uchokozi wa Juni 2025.

Aidha taarifa hiyo imesisitiza kuwa ukimya na kutojali huko ndiko kulikofungua njia ya kurudiwa kwa vita vingine vilivyolazimishwa mwezi Februari 2026, na kwamba wale waliokaa kimya wanapaswa kuwajibishwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *