Seattle, Marekani. Timu za taifa za Misri na Senegal, zimelazimika kuondoa nyota zilizokuwa katika jezi zao baada ya Shirikisho la Soka la Duniani (FIFA) kuzilazimisha kufanya mabadiliko hayo siku chache kabla ya michezo yao ya kwanza ya makundi ya Kombe la Dunia 2026.

Kwa mujibu wa FIFA, alama za nyota juu ya nembo ya timu za taifa wakati wa mashindano ya Kombe la Dunia inapaswa kuwakilisha tu mataji ya mashindano hayo na si mafanikio ya mashindano ya mabara.

Uamuzi huo umeathiri moja kwa moja mataifa kadhaa ya Afrika yenye historia kubwa ya mafanikio katika mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).

Nyota wa timu ya Taifa ya Misri, Mohamed Salah. Picha na Mtandao

Misri, mabingwa mara saba wa mashindano ya AFCON, wamelazimika kuondoa nyota saba walizokuwa wameziweka kuonyesha idadi ya mataji hayo ya Afrika.

Mbali na hilo, Misri pia imelazimika kubadili rangi ya namba za wachezaji kutoka rangi ya dhahabu na kuweka rangi nyeupe ili kuboresha muonekano kwenye matangazo ya televisheni.

Kwa upande wa Senegal, imejikuta pia ikilazimika kufanya marekebisho kama hayo baada ya FIFA kusisitiza kuwa nyota zinapaswa kuonyesha tu ubingwa wa Dunia.

Senegal ilikuwa imepanga kutumia nyota kuwakilisha mafanikio iliyoyapata kwenye michuano ya AFCON, lakini mchakato huo uliingia dosari kufuatia mzozo wa fainali ya AFCON 2025, ambapo Senegal licha ya kushinda uwanjani kwa bao 1-0, ilipokonywa ubingwa mezani kwa kudaiwa iliondoka uwanjani kabla ya mechi kukamilika baada ya kugoma katika mechi hiyo na kurejea uwanjanj, hatua iliyosababisha CAF kuipa ushindi Morocco.

Nyota wa timu ya Taifa ya Senegal, Sadio Mane. Picha na Mtandao

Hali hiyo imefanya msambazaji wao wa vifaa vya michezo, Puma kuendelea na muundo wa jezi zenye nyota moja ya taji la 2021 pekee.

Hata hivyo, timu zote mbili tayari zimeshaondoa alama za nyota hizo huku zikijiandaa na michezo yao ya kwanza katika makundi ya Kombe la Dunia.

Misri itashuka dimbani kesho Jumatatu, Juni 15, 2026 katika mechi yake ya kwanza dhidi ya Ubelgiji wakati Senegal itavaana na Ufaransa, Jumanne Juni 16.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *