Chanzo cha picha, Getty Images
Marekani na Iran zimetangaza kufikia makubaliano ya awali ya kumaliza vita kati yao, kumaliza miezi ya mvutano uliotikisa Mashariki ya Kati.
Maafisa kutoka pande zote mbili walisema Jumapili kuwa wamekubaliana juu ya mfumo wa makubaliano ambao pia unajumuisha pia kufunguliwa tena kwa Mlango-Bahari wa Hormuz, njia muhimu inayopitisha sehemu kubwa ya mafuta ya dunia.
Rais wa Marekani, Donald Trump, alitangaza mafanikio hayo kupitia mtandao wake wa Truth Social.
“Makubaliano na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sasa yamekamilika,” Trump aliandika.
Tangazo hilo lilikuja muda mfupi baada ya Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif, ambaye nchi yake imekuwa mpatanishi katika mazungumzo hayo, kusema makubaliano yalifikiwa mapema Jumatatu kwa saa za eneo hilo.
Maelezo kamili ya makubaliano hayo hayajatangazwa mara moja. Sharif alisema kupitia mtandao wa X kwamba makubaliano hayo yanataka:
“Kukomeshwa mara moja na kwa kudumu kwa operesheni zote za kijeshi katika maeneo yote ya mapigano, ikiwemo Lebanon.”
Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran nalo lilithibitisha kuwa shughuli zote za kijeshi katika maeneo yote ya mzozo, ikiwemo Lebanon, zitasitishwa kuanzia Jumatatu usiku.
Trump alisema kuwa Mlango wa Bahari wa Strait of Hormuz, ambao ni njia muhimu ya usafirishaji wa mafuta na gesi duniani na ambao Iran imekuwa ikidhibiti kwa miezi kadhaa, utafunguliwa tena Ijumaa.
Trump aliandika:
“Meli za dunia, washeni injini zenu. Mafuta yaanze kutiririka!”