
Viongozi mbalimbali duniani wamekaribisha hati ya makubaliano (MoU) kati ya Iran na Marekani, ambayo inahitimisha mara moja vita vya kichokozi vilivyoanzishwa na Marekani na Israel dhidi ya Iran, kuondoa mzingiro wa baharini, na kufungua tena Lango Bahari la Hormuz kwa usafiri wa kimataifa.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameyataja makubaliano hayo kuwa ni “hatua muhimu” kuelekea kutatuliwa kwa mgogoro huo.
Katika taarifa yake amebainisha matumaini kuwa pande husika zitajenga juu ya msukumo huu mpya na kuongeza juhudi zao ili kufikia suluhu ya mwisho ya mgogoro huu.
Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar, Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al Thani, amesema Qatar “inakukaribisha makubaliano hayo” na akaishukuru Pakistan kwa juhudi zake za upatanishi, akieleza matumaini kwamba pande zote zitashiriki mazungumzo yajayo “kwa roho chanya na ya kujenga.”
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesema anaona makubaliano hayo kuwa “maendeleo muhimu katika kuimarisha amani na utulivu katika eneo letu,” na akayakaribisha kwa kuridhika. Pia alitoa wito wa kuepuka uchochezi wowote unaoweza kuongeza mvutano kabla ya kutiwa saini kwa makubaliano hayo, huku akizishukuru Pakistan, Qatar na Saudi Arabia kwa mchango wao.
Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na Italia kwa pamoja zilitoa taarifa zikisema ziko “tayari kuondoa baadhi ya vikwazo husika endapo Iran itachukua hatua wazi na zinazoweza kuthibitishwa kuhusu mpango wake wa nyuklia,” na kuongeza kuwa zitafanya kazi kwa karibu na pande zote ili kufikia suluhu ya kidiplomasia ya muda mrefu.
Waziri Mkuu wa Japan Sanae Takaichi amesema Japan “ina matumaini makubwa” kwamba makubaliano ya mwisho kuhusu suala la nyuklia la Iran yatafikiwa hivi karibuni.
Waziri Mkuu wa Australia Anthony Albanese pia amekaribisha makubaliano hayo, akisema Australia kwa muda mrefu imekuwa ikitoa wito wa kupunguzwa kwa mvutano na kumalizwa kwa mgogoro huo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa New Zealand Winston Peters ameyataja makubaliano hayo kuwa “ya kihistoria na yenye kujenga,” akisisitiza kwamba “mazungumzo na diplomasia ndizo njia bora zaidi za kushughulikia migogoro ya muda mrefu.”