
ARUSHA: SERIKALI itaendelea kuongeza nguvu katika uhifadhi wa wanyamapori aina ya faru ambao wapo haratini kutoweka kwa kuimarisha Mradi wa Kimkakati wa Uhifadhi wa Faru Weupe ili kuongeza chachu ya ongezeko la uhifadhi na utafiti wa wanyamapori waliopo nchini.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamad Hasaan Chande wakati wa hafla maalumu ya kuwaachilia huru faru weupe 17 waliopo kwenye Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro ikiwa ni mradi maalumu uliofadhiliwa kupitia Shirika la Andbeyond kwa ushirikiano na Serikali ya Afrika Kusini
“Kwa kweli mmebuni kitu kizuri ambacho kinaleta tija na ufanisi na kuleta lmaendeleo kwa nchi yoyote, lengo kuu ikiwa ni kuongeza utafiti, uhifadhi na kupata elimu.
“Wako wengi duniani watakuja kujifunza kupitia Faru hawa weile wakiwa ama ni wanafunzi, au wakufunzi,” Chande.
Amempongeza na kumshukuru mhifadhi namba moja nchini katika uhifadhi na muongoza watalii, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa utayari na utashi wake katika uhifadhi huku akiishukuru pia Serikali ya Afrika Kusini kwa ushirikiano mzuri na Tanzania kwa ufadhili wa faru hao.
Kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mkurugenzi wa Wanyamapori wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Alexander Lobora amesema hatua ya kuwaachia huru Faru hao kutoka kwenye uzio imesaidia katika kuongeza wigo wa kupata eneo kubwa zaidi la kujitafutia malisho huku wakihakikishiwa ulinzi kutokana na miundombinu ya ufuatiliaji wa wanyama ndani ya hifadhi.
“Kwa niaba ya Sekta ya Utalii kwa ujumla serikali ipo tayari kupokea Faru zaidi kwa awamu ya pili kwa sababu tayari tumejifunza mengi kwa awamu ya kwanza na lengo la Faru hawa kubwa ni uhifadhi kama tulivyosaini Mikataba ya Kimataifa kama nchi kuhusu wanyamapori ambao wapo hatarini kutoweka,” alisema Dk. Lobora.
Kwa upande wake Kamishina wa Uhifadhi wa Mamalaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) Abdul-Razaq Badru amesema, NCAA itaendelea kuimarisha ulinzi mkali kwa kutumia mitambo ya kisasa katika kuwalinda na kuwahifadhi wanyama hao walio hatarini kutoweka kwa ajili ya manufaa ya taifa na kuongeza mwitikio wa uhifadhi na utafiti kwa kizazi hiki na kijacho.
Naye Mtendaji Mkuu wa Shirika la Anbeyond Bw. Mussa Mathayo amesema awali ulifanya utafiti wa eneo la kuishi Faru hao ili kuwa na afya njema na kujitafutia malisho na kubainisha kuwa shirika hilo lipo tayari kuongeza idadi ya Faru waliosalia ili kufikisha Faru 36 kama ilivyokuwa kwenye mkataba.