
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi amejadili makubaliano Iran na Marekani na wenzake wa Uturuki, Iraq, Misri, Japani na Saudi Arabia, akisisitiza wajibu wa Marekani wa kutekeleza makubaliano hayo.
Akizungumza kwa simu kwa nyakati tofauti mapema leo Jumatatu na Hakan Fidan wa Uturuki, Fuad Hussein wa Iraq, Badr Abdelatty wa Misri, Toshimitsu Motegi wa Japani na Faisal bin Farhan wa Saudi Arabia, Araqchi amejadili mchakato na vifungu vya hati ya makubaliano ya Islamabad.
Akiashiria wajibu wa Marekani wa kutekeleza makubaliano hayo, Araqchi amesisitiza haja ya kusitishwa kikamilifu hujuma zinazovuruga amani na mashambulizi ya Israel dhidi ya Lebanon.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pia ametoa shukrani kwa nafasi na mchango wa Uturuki, Iraq, na Misri katika kuunga mkono juhudi za kufikiwa makubaliano ya kusitisha mapigano, kupunguza mvutano na kufuatilia juhudi za kidiplomasia ili kupatikana utulivu na usalama wa kikanda.
Mawaziri wa mambo ya nje wa Iran, Uturuki, Iraq na Misri pia wamesisitiza kuendelezwa mashauriano ya karibu na ushirikiano kuhusu matukio ya kikanda na ulazima wa kuimarishwa juhudi za kidiplomasia ili kudumisha amani na utulivu.
Katika mazungumzo yake na mwenzake wa Japani, Araqchi amebainisha vifungu muhimu zaidi vya hati ya makubaliano hayo na kuelezea matumaini kwamba utekelezaji wake utaashiria mwanzo wa ukurasa mpya ya ushirikiano wa kiuchumi na uwekezaji kati ya nchi hizo mbili.
Araqchi pia amempa taarifa mwenzake wa Saudi Arabia kuhusu vifungu vya hati ya makubaliano ya Islamabad na kutoa shukrani kwa Saudi Arabia kwa mchango wake katika mchakato unaoendelea wa kidiplomasia unaolenga kukomesha uchokozi kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran na kuimarisha amani na usalama wa kikanda.
Haya yanakuja baada ya Sekretarieti ya Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran (SNSC) kuthibitisha kuwa Iran na Marekani zimekamilisha maandishi ya hati ya makubaliano (MoU) yanayolenga kumaliza vita, kusimamisha mara moja na daima operesheni zote za kijeshi katika nyanja zote, ikiwemo Lebanon, na pia kuondoa mzingiro wa baharini uliowekwa na Marekani dhidi ya Iran.
Sekretarieti hiyo imeongeza kuwa hati hiyo ya makubaliano inatarajiwa kutiwa saini rasmi siku ya Ijumaa, tarehe 19 Juni.