Dar es Salaam. Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa amesema Serikali ipo hatua za mwisho kuandaa mfumo imara wa kitaasisi na kisheria wa upandikizaji wa viungo utakaosaidia kuratibu huduma hizo kwa uwazi, uadilifu na usalama wa mgonjwa, mchangiaji pamoja na kuzingatia maadili ya kitabibu.

Amesema mfumo huo utaanzia hatua ya tathimini ya mgonjwa, maandalizi ya upasuaji, huduma wakati wa upasuaji na ufuatiliaji wa muda mrefu baada ya upandikizaji.

Waziri Mchengerwa ametoa kauli hiyo usiku wa jana Jumapili, Juni 14, 2026 jijini Dar es Salaam, katika hafla ya chakula cha usiku iliyoandaliwa mahsusi kuwapongeza vinara wa uchangiaji damu nchini.

Hatua hiyo ni sehemu ya kutambua mchango wao mkubwa katika kuokoa maisha ya wananchi na ilikuwa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mchangia Damu Duniani ya Juni 14, 2026.

Mchengerwa amesema nchi yenye mfumo imara wa damu salama ina uwezo mkubwa wa kutoa huduma za kibingwa kwa uhakika zaidi, akibainisha damu salama ni sehemu ya haki ya mgonjwa kupata huduma bora na salama.

“Ninawaelekeza wataalamu wetu kuhakikisha maandalizi ya mfumo huu wa upandikizaji yanaweka ubora kama msingi mkuu.”

Hospitali zitakazotoa huduma za upandikizaji wa viungo lazima ziwe na mfumo imara wa damu, kamati ya matumizi ya damu hospitalini, huduma bora za maabara, uwezo wa kuchakata na kuhifadhi mazao ya damu, pamoja na mfumo wa kutathmini changamoto zinapojitokeza,” amesema.

Ikumbukwe kwa mara ya kwanza aliyekuwa Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu mwaka 2023 alisema Serikali ipo katika mchakato wa kuandaa muswada wa kuruhusu watu kuchangia viungo vya ndani ikiwamo figo.

“Lakini sisi hatuna sheria nchini ya kuchangia viungo vya ndani, ndio tunataka kuitunga kwa hiyo tunahitaji kutoa elimu…unaweza ukatoa figo yako moja na ukaishi vizuri tu,” alisema Ummy wakati anazindua jengo la Mkemia Mkuu wa Serikali jijini Dodoma.

Sheria hiyo itaweka utaratibu ni nani atoe viungo na nani hawezi kutoa viungo. Misingi ya Shirika la Afya Duniani (WHO) inakataza ufanyaji wa biashara ya viungo sawa na uchangiaji wa damu ambao mtu anayechangia huchangia kwa ajili ya kumsaidia muhitaji na si kufanya biashara.

Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, wakati akizungumza katika hafla iliyofanyika usiku wa jana Jumapili, Juni 14, 2026 jijini Dar es Salaam iliyoandaliwa mahsusi kuwapongeza vinara wa uchangiaji damu nchini.

Kuhusu TMDA

Katika hatua nyingine, Mchengerwa amesema Serikali inatambua umuhimu wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) katika usimamizi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi.

Kutokana na hilo, amesema kanuni na mifumo ya TMDA ya kusimamia na kudhibiti damu pamoja na mazao yake ipo hatua za mwisho za kukamilishwa.

Amesema kanuni hizo zinalenga kuweka msingi thabiti wa kisheria katika ukusanyaji, upimaji, uchakataji, uhifadhi, usambazaji, ufuatiliaji wa usalama na uwajibikaji wa kila mdau anayehusika katika mnyororo wa damu salama.

“Katika kuimarisha udhibiti wa damu na mazao ya damu, tunaongeza ulinzi wa kisheria kwa maisha ya Watanzania. Kanuni zinazoandaliwa ni daraja kati ya nia njema na mfumo unaowajibika.”

“Tunaweka mfumo ambao kila tone la damu litafuatiliwa, kila hatua itaweza kuthibitishwa na kila muhusika kuwajibika, hii ndiyo maana ya kusema Tanzania tunayoijenga si ya kufuata viwango tu, bali ya kuweka viwango vinavyoheshimika,” amesema.

Baadhi ya wadau mbalimbali waliohudhuria hafla ya chakula cha jioni ya kuwapongeza wachangiaji wa damu jijini Dar es Salaam

Mahitaji ya damu

Akizungumzia mahitaji ya damu, Mchengerwa amesema damu inahitajika zaidi kwa wagonjwa wa saratani, huduma za kibingwa na ubingwa bobezi, maandalizi ya matibabu mbalimbali pamoja na waathirika wa ajali.

Amesema kuichangia damu ni sadaka ya kurejesha uhai wa mtu mwingine, hivyo damu ni fursa muhimu ya kuokoa maisha.

“Damu salama ni msingi wa matibabu na huduma za kibingwa. Upandikizaji wa figo, uloto, upasuaji wa moyo, matibabu ya saratani na huduma kwa waathirika wa ajali haziwezi kufanyika bila mfumo imara wa damu salama, mazao ya damu, vipimo sahihi na uhifadhi bora. Upandikizaji salama unahitaji damu salama,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *