Dar es Salaam. Ujio wa mtoto wa kiume wa msanii Whozu na mwigizaji Wema Sepetu umeendelea kuibua hisia kwa watu mbalimbali. Huku mtangazaji wa redio na televisheni, Diva Malinzi maarufu kama Diva The Bawse, akisema tukio hilo limempa matumaini kuwa siku moja naye atapata mtoto.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram Diva ameandika ujumbe ulioonyesha jinsi alivyoguswa na taarifa za Wema kujifungua mtoto baada ya miaka mingi ya kusubiri kutimiza ndoto ya kuwa mama.

“Na mimi kuna siku nitapata mtoto. Nimeamini kweli usikate tamaa katika haya maisha. Nimeamini kwenye wakati wa Mungu. Nimefurahia mtoto wa Wema mpaka nimelia,” ameandika Diva.

Ujumbe huo umewagusa mashabiki wake wengi waliomiminika katika sehemu ya maoni wakimtakia heri na kumtia moyo aendelee kuwa na imani.

Kauli ya Diva imekuja wakati furaha ya ujio wa mtoto wa Wema ikiendelea kutawala katika mitandao ya kijamii. Kwa muda mrefu, Wema amekuwa akizungumzia wazi tamanio lake la kupata mtoto, huku akikabiliwa na changamoto mbalimbali na wakati mwingine maneno ya kukatisha tamaa kutoka kwa baadhi ya watu.

Kwa wengi, ujio wa mtoto huyo aliyezaliwa Ijumaa Juni 12,2026 umeonekana kuwa ushuhuda wa subira, matumaini na kuamini kuwa kila jambo lina wakati wake.

Hata hivyo, kauli ya Diva haijaja kwa bahati mbaya. Mwaka 2023, mtangazaji huyo aliweka wazi changamoto anazopitia katika safari yake ya kutafuta mtoto.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati huo, alisema amekuwa akipata ujauzito lakini mara kadhaa umekuwa ukiharibika kutokana na changamoto za kiafya zilizotokana na upasuaji aliowahi kufanyiwa.

“Ninapenda watoto na natamani kuwa mama. Nimekuwa nikipata changamoto katika safari hiyo. Kuna wakati naona matumaini makubwa ya kupata mtoto lakini katikati mambo yanabadilika. Hata hivyo, bado ninaendelea na matibabu na namshukuru Mungu kwa sababu naona hatua za maendeleo,” alisema Diva.

Alieleza kuwa pamoja na kuendelea na matibabu, aliwahi kufikiria uwezekano wa kutafuta huduma za matibabu nje ya nchi ili kuongeza nafasi ya kutimiza ndoto yake ya kupata mtoto.

Mbali na hilo, Diva alisema kwa muda mrefu amekuwa na hamu ya kuasili mtoto(adaption). Lakini alidai kuwa taratibu za kufanya hivyo nchini zimekuwa na changamoto zinazohitaji muda na kufuata hatua mbalimbali za kisheria.

Kwa mujibu wa Diva, upendo wake kwa watoto umejidhihirisha hata katika shughuli mbalimbali za kijamii alizowahi kuzifanya, ikiwemo kusaidia watoto wenye mahitaji maalumu ya matibabu.

Sasa, baada ya kushuhudia kile alichokiita furaha ya Wema kuwa mama, Diva amesema ameendelea kupata nguvu mpya za kuamini kuwa ndoto yake pia itatimia siku moja ya kushika mimba na kuitwa mama.

Baadhi ya mashabiki wametumia nafasi hiyo kumtia moyo Diva kuendelea kuwa na imani. Mfuasi mmoja alimtia moyo kwa kumwambia “You are the next. Mungu anakupenda sana, endelea kumwamini tu. Yeye ni Baba wa rehema. Usife moyo dada. Mungu wetu ni Baba mzuri mno.”

Shabiki huyo pia amenukuu andiko la Isaya 41:10 linalosema: “Usiogope kwa maana mimi nipo pamoja nawe, usifadhaike kwa maana mimi ni Mungu wako; nitakutia nguvu, naam nitakusaidia, naam nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu.”

Ujumbe huo ni miongoni mwa mamia ya maoni yaliyojitokeza chini ya chapisho la Diva, wengi wakimtakia heri na kumtia moyo aendelee kuwa na matumaini katika safari yake ya kutimiza ndoto ya kuwa mama.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *