
Dar es Salaam. Kamati ya Bunge ya Bajeti, imetaka kiasi cha Sh200 bilioni kilichotolewa na Serikali kwa ajili ya maendeleo ya vijana kisigawanywe katika wizara mbalimbali kama inavyofanyika, bali kiachwe kwenye wizara inayohusika na kundi hilo.
Hata hivyo, Rais Samia Suluhu Hassan, aliwahi kueleza uamuzi wa kuzigawanya fedha hizo unafuatana na sekta zilizolengwa kuwanufaisha vijana ambapo za kilimo zinatekelezwa na Wizara ya Kilimo, Uvuvi chini ya Wizara ya Uvuvi na nyingine.
Maoni kama ya kamati hiyo, yamewahi kutolewa na Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ya Chama cha ACT Wazalendo, Abdul Nondo, aliyetaka Serikali iache fedha hizo zibaki katika wizara maalumu ya vijana, ili kurahisisha uratibu na usimamizi wake.
Aidha, wabunge wakati wakichangia Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu ya mwaka 2026/27 pamoja na Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais- Maendeleo ya Vijana waligusia suala hilo wakitaka fedha hizo zisigawanywe bali wizara ya vijana ndiyo ipewe jukumu ya kuzisimamia.
Wabunge walisema kuzigawa wizara mbalimbali kutasababisha walengwa kutofikiwa kwani usimamizi hautakuwa mzuri.
Leo, Jumatatu Juni 15, 2026 na Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Mashimba Ndaki, alipowasilisha tathimini ya mwenendo wa viashiria vya uchumi jumla kwa mwaka 2025/26 amegusia suala hilo.
Katika kujenga hoja hiyo, amesema kamati imebaini zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania wanajihusisha na shughuli zilizopo kwenye sekta isiyo rasmi, hususan kilimo cha kujikimu, huku sekta rasmi ikichukua takribani asilimia 20 hadi asilimia 25.
Amesema zaidi ya vijana 800,000 huingia katika soko la ajira kila mwaka, lakini sekta rasmi haina uwezo wa kuwaajiri wote ambapo katika kipindi cha mwaka 2023/24 hadi 2024/25 ajira katika sekta rasmi ziliongezeka kwa wastani wa ajira 354,702.
Hali hiyo, amesema inachangia ukosefu wa ajira hususan kwa vijana na wanawake na kukithiri kwa sekta isiyo rasmi kwa mujibu wa taarifa ya Benki ya Dunia ya 2025.
“Kutokana na changamoto hizo, kamati inashauri Sh200 bilioni zilizotolewa kwa wizara inayoshughulikia maendeleo ya vijana kisigawanywe kwenye wizara mbalimbali kama inavyofanyika hivi sasa, badala yake fedha hizo zibaki kwenye wizara yenye dhamana ili kuratibu masuala yote yanayohusu vijana,” amesema.
Pia, amesema Serikali inapaswa kuwekeza katika sekta zinazoajiri nguvu kazi nyingi kama kilimo biashara, utalii na viwanda vidogo.
Amesema kamati inapendekeza Serikali iimarishe elimu ya ufundi na ufundi stadi ili kuwaandaa vijana wawe tayari kwa ajira rasmi katika viwanda na sekta zinazotumia teknolojia ya kisasa.
Pendekezo lingine la kamati hiyo ni kuunganisha mifuko ya uwezeshaji ya vijana iliyopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Mfuko wa SELF ulio chini ya Wizara ya Fedha ili kutoa mikopo kwa wanawake na vijana chini ya Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana.
“Kurasimisha sekta isiyo rasmi kwa kurahisisha usajili wa biashara na kutoa motisha kwa biashara ndogo na za kati kuingia kwenye sekta rasmi,” amesema.