Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA), Philippe Lazzarini, ametahadharisha kwamba utawala wa kizayuni wa Israel inaonekana unapanga kufanya “mauaji ya halaiki ya idadi kubwa” katika Mji wa Ghaza huku ukiwa unashadidisha mzingiro wake na mashambulizi makubwa ya kijeshi dhidi ya mji huo.

Lazzarini ametoa indhari hiyo baada ya utawala wa kizayuni kutoa vitisho kwa wakazi wote wa Mji wa Ghaza kwamba, Wapalestina watakaosalia katika mji huo watahesabiwa kuwa “magaidi” au “wafuasi wa magaidi.”

Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amesema, matamshi hayo yanazua hofu ya kufanyika mauaji ya umati.

“[Hii] ni taarifa inayoashiria kufanyika mauaji yaliyokwisha pangwa ya idadi kubwa ya watu: kuzidi kuua wanawake, watoto, wazee na watu wanaoweza kudhuriwa kirahisi ambao hawawezi kuhama”, ameeleza mkuu huyo wa UNRWA.

Lazzarini amesisitiza kuwa, hakuna mamlaka yoyote yenye “kibali cha kuua raia” na akaonya kwamba kuendelea hali iliyopo ya kutochukuliwa hatua yoyote kunaweza kupelekea kuwa washiriki wa kile ambacho wachunguzi wa Umoja wa Mataifa tayari wameshakitangaza kuwa ni mauaji ya kimbari.

Matamshi hayo ya Mkuu wa shirika la UNRWA yametolewa wakati Ghaza inaendelea kuandamwa na mashambulizi makali ya makombora na mabomu ya jeshi la utawala wa kizayuni sambamba na kuwekewa mzingiro na jeshi hilo.

Kwa mujibu wa tovuti ya habari ya The New Arab, Wapalestina wapatao 600,000 wamebaki wamekwama katika Mji wa Ghaza unaoshambuliwa vikali na jeshi la utawala ghasibu wa Israel.

Hii ni katika hali ambayo, idadi ya Wapalestina wanaouawa shahidi kutokana na vita vya kinyama na mauaji ya kimbari yanayofanywa na jeshi la kizayuni inazidi kuongezeka kila siku.

Wizara ya Afya ya Ghaza imeripoti Wapalestina wasiopungua 66,225 wameshauawa hadi sasa na wengine zaidi ya 168,000 wamejeruhiwa tangu Israel ilipoanzisha vita dhidi ya Ghaza Oktoba 2023.

Uchunguzi wa kujitegemea unaonyesha kuwa idadi halisi ya vifo inaweza ikawa ni zaidi ya 100,000…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *