
Serikali ya Kenya imewahakikishia raia wake wanaofanya biashara nchini Tanzania kwamba hawataguswa na agizo jipya la leseni lililotolewa hivi karibuni na serikali ya Tanzania.
Kauli hiyo inafuatia hali ya wasiwasi iliyoibuka awali baada ya chapisho la Leseni za Biashara, la Julai 28, 2025, linalozuia raia wa kigeni kufanya baadhi ya biashara nchini Tanzania.
Kufuatia agizo hilo, Nairobi ilifanya majadiliano na Dar es Salaam ikidai kwamba, agizo hizo linakwenda kinyume na itifaki ya soko la pamoja la Afrika Mashariki, ambayo inatoa hakikisho kwa watu kusafiri bila pingamizi, kupata huduma, na kuwa na haki ya kufanya biashara katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC.
Katika taarifa aliyotoa leo Ijumaa, Dkt. Caroline Karugu, ambaye ni Katibu Mkuu katika Idara ya Masuala ya Afrika Mashariki amesema, kufuatia majadiliano ya pamoja, Tanzania imeihakikishia Kenya kwamba agizo hilo halitawaathiri raia wake.
“Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeripoti kuwa, mpaka sasa hakuna biashara ya Mkenya iliyoathirika kufuatia agizo hilo na kuhakikisha kwamba hakuna biashara ya Mkenya itakayoathirika hata kwa siku za baadae,” amesema Dkt Karugu.
Dkt. Karungu amewataka Wakenya waliopo nchini Tanzania kuendelea na shughuli zao bila hofu, na kuwataka wawasiliane na Ubalozi wa Kenya uliopo nchini Tanzania iwapo kutakuwa na changamoto yoyote.
Wakati huo huo, Kenya imeeleza kufurahishwa na hatua hiyo ya serikali ya Tanzania, na kusema kwamba, inaonesha utashi wa ushirikiano ndani ya EAC…/