DAR ES SALAAM; SAA 12 alfajiri, wakati taa za magari bado zinang’aa katika baadhi ya mitaa ya Dar es Salaam na sehemu kubwa ya jiji ikiwa haijaamka, maisha tayari yameanza juu ya Daraja la Tanzanite.

Upepo mwanana kutoka Bahari ya Hindi unapuliza taratibu. Chini yake, mawimbi yanakatiza kwa utulivu. Juu yake, mamia ya watu wameanza kujaza njia za watembea kwa miguu. Wengine wanakimbia. Wengine wanatembea kwa hatua za utulivu.

Waendesha baiskeli nao wanapita kwa kasi huku wakifurahia mandhari ya bahari inayolizunguka daraja hilo pande zote mbili.

Miongoni mwao yupo Aaron, mkazi wa Kawe, kama ilivyo kwa mamia ya wengine, mwisho wa wiki wake huanza hapa.

“Hapa ni sehemu nzuri ya mazoezi. Unapata hewa safi, mazingira mazuri na usalama. Kila wiki lazima nije,” anasema huku akijiandaa kuanza mbio zake za asubuhi.

Wakazi hao hawafiki hapo kwa bahati mbaya.

Kwa utaratibu unaosimamiwa na TANROADS, kila Jumamosi Daraja la Tanzanite hufungwa kwa magari, pikipiki na bajaji kuanzia saa 12 alfajiri hadi saa 9 asubuhi ili kutoa nafasi kwa wananchi kufanya mazoezi katika mazingira salama.

Katika muda huo, daraja hubadilika kutoka njia ya usafiri na kuwa uwanja mkubwa wa wazi unaowakutanisha wakimbiaji, watembea kwa miguu, waendesha baiskeli na familia kutoka maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam.

Mtendaji Mkuu wa TANROADS Mhadisi Mohamed Besta anasema hatua hiyo imeonesha namna mradi uliobuniwa kutatua changamoto za usafiri ulivyogeuka kuwa sehemu ya ustawi wa jamii.

“Awali lengo kuu lilikuwa kuboresha mtiririko wa magari. Leo tunaona mamia ya wananchi wakilitumia kwa ajili ya mazoezi, afya na shughuli za kijamii. Hii ni thamani ya ziada ambayo haikuwa rahisi kuipima wakati wa kuanza kwa mradi,” anasema.

Mita chache kutoka alipo Aaron, Benedicto Makwisa anafungua biashara yake ya madafu.

Anasema kabla ya eneo hili kuwa maarufu kwa watembea kwa miguu na wanamichezo, hakuwahi kufikiria angeweza kupata wateja wengi kiasi hicho.

“Siku nzuri naweza kuuza madafu zaidi ya 100. Watu wakimaliza mazoezi wengi hupitia hapa,” anasema.

Darala la Tanzanite Dar es Salaam. (Picha na maktaba).

Kwa Aaron, Daraja la Tanzanite ni sehemu ya kujenga afya.

Kwa Benedicto, ni chanzo cha kipato.

Kwa Dar es Salaam, ni alama mpya ya jiji.

Lakini kwa Tanzania, daraja hilo limekuwa ushahidi wa namna uwekezaji wa kimkakati katika miundombinu unavyoweza kubadilisha maisha ya wananchi kwa njia zinazozidi lengo la awali la mradi.

Kwa mujibu wa TANROADS, Daraja la Tanzanite lenye urefu wa kilometa 1.03 pamoja na barabara zake unganishi za kilometa 5.2 lilijengwa kwa gharama ya takribani Shilingi bilioni 243.

Mradi huo ulitekelezwa ili kupunguza msongamano wa magari katika moja ya maeneo yenye shughuli nyingi zaidi jijini Dar es Salaam.

TANROADS inaeleza kuwa kabla ya daraja hilo kujengwa, wastani wa magari zaidi ya 52,000 yalikuwa yakipita katika eneo hilo kila siku, hali iliyochangia msongamano mkubwa wa magari katika Barabara ya Ali Hassan Mwinyi na Daraja la Selander.

Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa akishiriki mazoezi pamoja na baadhi ya wanamichezo eneo la Daraja la Tanzanite.

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega anasema ongezeko la shughuli za kiuchumi na makazi katika eneo la Peninsula lilikuwa limeongeza shinikizo kubwa kwa miundombinu iliyokuwepo.

“Mahitaji ya usafiri yalikuwa yanaongezeka kwa kasi. Daraja la Tanzanite lilijengwa kama suluhisho la muda mrefu la kuboresha mtiririko wa magari na kuongeza ufanisi wa mtandao wa barabara wa Dar es Salaam,” anasema.

Kwa miaka mingi, wakazi wa Oysterbay, Masaki, Kawe na maeneo mengine ya Peninsula walikabiliwa na changamoto ya foleni katika safari zao za kila siku.

Leo hali hiyo imebadilika kwa kiasi kikubwa. Lakini mafanikio ya Daraja la Tanzanite hayaishii kwenye magari yanayopita juu yake.

Yanaonekana pia kwa watu wanaolitumia. Yanaonekana katika biashara zinazochipuka kandokando yake. Na yanaonekana katika taswira mpya ya Dar es Salaam inayojitokeza mbele ya macho ya wageni na wakazi wake.

Daraja hilo limekuwa moja ya alama mpya za maendeleo ya miundombinu nchini.

Akilizindua Daraja la Tanzanite, Rais Samia Suluhu Hassan alisema Serikali itaendelea kuwekeza katika miundombinu ya kimkakati ili kurahisisha usafiri, kupunguza gharama za biashara na kufungua fursa mpya za kiuchumi kwa wananchi.

Miaka michache baadaye, utekelezaji wa miradi mbalimbali nchini unaonyesha namna dira hiyo ilivyotafsiriwa katika vitendo.

Hata hivyo, ili kuelewa umuhimu wake kikamilifu, ni lazima kuliangalia kama sehemu ya simulizi kubwa zaidi ya mabadiliko yaliyotokea katika sekta ya ujenzi ndani ya miaka mitano iliyopita.

Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Ujenzi, mwaka 2021 Tanzania ilikuwa na kilometa 10,830.2 za barabara za lami katika mtandao wa barabara za kitaifa.

Kufikia mwaka 2026, mtandao huo umeongezeka hadi kilometa 12,225.26.

Hii ni ongezeko la kilometa 1,395 za barabara za lami ndani ya kipindi cha miaka mitano.

Kwa lugha rahisi, ni sawa na kujenga mtandao mpya wa barabara za lami wenye urefu unaoweza kuunganisha Dar es Salaam na Dodoma zaidi ya mara mbili.

Ukuaji huo umeenda sambamba na upanuzi wa mtandao wa TANROADS uliofikia kilometa 37,734.41 mwaka 2026.

Mhandisi wa TANROADS, Zuhura Amani, anasema mtandao huo ndio uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania.

“Mtandao huo ndio unaosaidia mazao ya wakulima kufika masokoni.” “Ndimo bidhaa za viwandani husafirishwa kwenda bandari, Ndimo watalii husafiri kuelekea hifadhi za taifa na ndimo wananchi husafiri kufuata huduma za afya, elimu na biashara.”

Barabara ya Chunya-Makongolosi

Kwa mujibu wa Wizara ya Ujenzi, Serikali pia imefanikiwa kujenga madaraja makubwa 18 katika kipindi cha miaka mitano ya Awamu ya Sita.

Madaraja hayo yamejengwa katika maeneo mbalimbali yaliyokuwa yakikabiliwa na changamoto za vivuko, mafuriko au kukatika kwa mawasiliano wakati wa mvua.

Daraja la Tanzanite limekuwa sura inayotambulika zaidi ya mafanikio hayo.

Lakini nyuma yake kuna madaraja mengine yanayoendelea kubadilisha maisha ya wananchi.

Miongoni mwao ni Daraja la Pangani mkoani Tanga.

Kwa mujibu wa TANROADS, daraja hilo lenye urefu wa mita 525 limefikia takribani asilimia 70 ya utekelezaji.

Mara litakapokamilika, litakuwa sehemu muhimu ya barabara inayounganisha Dar es Salaam, Bagamoyo, Tanga, Horohoro na Mombasa.

Kwa wataalamu wa uchumi, miradi kama hiyo ni zaidi ya miundombinu ya usafiri.

Ni uwekezaji katika ukuaji wa uchumi. Ni uwekezaji katika biashara. Na ni uwekezaji katika ushindani wa taifa.

Mchumi Ally Mkimo anaamini kuwa miundombinu bora ni moja ya silaha muhimu katika kupunguza gharama za kufanya biashara.

Anasema kila saa inayookolewa barabarani, kila kilometa ya lami inayoongezwa na kila daraja linaloondoa kikwazo cha usafiri huongeza ufanisi wa uchumi.

“Miundombinu si suala la barabara pekee. Ni suala la uzalishaji, biashara na uwekezaji. Nchi inayowekeza katika miundombinu inawekeza katika ukuaji wake wa baadaye,” anasema.

Kauli hiyo inaonekana wazi katika simulizi la Benedicto.

Anapowauzia madafu wakimbiaji, waendesha baiskeli na watembea kwa miguu wanaotembelea Daraja la Tanzanite kila wiki, anaona moja kwa moja namna mradi wa ujenzi unavyoweza kuzaa shughuli nyingine za kiuchumi.

“Hawa wote ni wateja ambao awali hawakuwepo. Sasa eneo hili limekuwa maarufu sana,” anasema.

Wataalamu wa maendeleo mara nyingi huita matokeo hayo “athari zisizo za moja kwa moja za miundombinu”.

Ni matokeo ambayo hayaandikwi kwenye michoro ya wahandisi lakini hujitokeza baada ya mradi kukamilika.

Katika mwaka wa fedha 2025/26 pekee, zaidi ya Shilingi trilioni 1.319 zilikuwa zimetolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo chini ya Wizara ya Ujenzi hadi Machi 2026.

Kwa mujibu wa taarifa ya utekelezaji wa wizara hiyo, fedha hizo zilikuwa sawa na asilimia 72.8 ya bajeti yote ya maendeleo iliyoidhinishwa kwa mwaka huo wa fedha.

Fedha hizo ziliwezesha kukamilika kwa kilometa 206.33 za barabara za lami pamoja na madaraja makubwa manne.

Aidha, miradi 76 kati ya 81 ya madaraja ya dharura yaliyoathiriwa na mvua za El Niño ilikamilishwa.

Haya si mafanikio ya kawaida.

Ni ushahidi wa uwezo wa kuhamisha fedha kutoka kwenye vitabu vya bajeti kwenda kwenye miradi inayotumiwa na wananchi.

Lakini nyuma ya mafanikio hayo kuna suala jingine muhimu; ushiriki wa wataalamu na makandarasi wazawa.

Kwa miaka mingi, sehemu kubwa ya miradi mikubwa ya miundombinu ilitekelezwa na kampuni za nje.

Hata hivyo, Serikali imeendelea kusisitiza ongezeko la ushiriki wa makandarasi wa ndani katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Rais wa Chama cha Makandarasi Wanawake Tanzania, Mhandisi Judith Odunga, anaamini ushiriki wa wazawa katika miradi mikubwa ni uwekezaji wa muda mrefu katika uwezo wa taifa.

“Kila mradi unaotekelezwa kwa ushiriki wa makandarasi wa ndani unaacha maarifa, uzoefu na uwezo ambao unabaki nchini. Huo ndiyo msingi wa kujenga sekta imara ya ujenzi kwa kizazi kijacho,” anasema.

Lengo ni kuhakikisha kuwa pamoja na kujenga miundombinu, Tanzania pia inajenga uwezo wa kitaalamu wa wahandisi, wakandarasi na washauri wake.

Faida za mkakati huo zinaonekana wazi. Kila mradi unaotekelezwa kwa ushiriki mkubwa wa wataalamu wa ndani huongeza ajira. Hujenga uzoefu.

Na huandaa kizazi kipya cha wataalamu wa sekta ya ujenzi.

Lakini pengine athari kubwa zaidi ya Daraja la Tanzanite haionekani katika nguzo zake, nyaya zake au saruji iliyotumika kulijenga.

Inaonekana katika afya za wananchi.

Kila mwisho wa wiki mamia ya wakazi wa Dar es Salaam hulitumia daraja hilo kufanya mazoezi.

Kwa wengi ni sehemu ya kawaida ya ratiba zao.

Kwa wataalamu wa afya, ni sehemu ya mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza.

Miongoni mwa wanaotumia daraja hilo kufanya mazoezi ni Rehema Magesa, mkazi wa Mikocheni.

“Sasa tunakuja hapa kama familia. Ni eneo salama, lenye mandhari nzuri na linawahamasisha watu wengi kufanya mazoezi,” anasema.

Barabara ya Njombe-Makete

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, zaidi ya asilimia 34 ya vifo vinavyotokea nchini vinahusishwa na magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo kisukari, shinikizo la damu, saratani, magonjwa ya moyo na magonjwa ya figo.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha kuwa magonjwa yasiyoambukiza husababisha zaidi ya vifo milioni 41 duniani kila mwaka na ndiyo chanzo kikuu cha vifo duniani.

Katika mazingira hayo, uwepo wa eneo salama linalowezesha wananchi kutembea, kukimbia na kuendesha baiskeli una umuhimu unaozidi thamani ya fedha zilizotumika kulijenga.

Aaron anaamini hilo. “Ukija hapa asubuhi utakuta watu wa rika zote. Vijana, wazee, wanawake na watoto. Watu wengi wamehamasika kufanya mazoezi,” anasema.

Kauli yake inaonyesha ukweli mmoja muhimu. Maendeleo ya taifa hayawezi kutenganishwa katika sekta moja pekee. Barabara zinahusiana na biashara. Biashara zinahusiana na ajira.

Ajira zinahusiana na ustawi wa wananchi. Na ustawi wa wananchi unahusiana na afya.

Daraja la Tanzanite limeonyesha jinsi miundombinu inaweza kugusa maeneo yote hayo kwa wakati mmoja. Leo hii, daraja hilo linaonekana kama moja ya alama kuu za Dar es Salaam.

Lakini maana yake halisi ipo mbali zaidi ya mwonekano wake. Ipo katika muda unaookolewa na maelfu ya watumiaji wa barabara kila siku. Ipo katika biashara zinazozaliwa kandokando yake.

Ipo katika wananchi wanaolifanya kuwa sehemu ya maisha yao ya kila wiki. Na ipo katika ujumbe wake mkubwa zaidi; kwamba uwekezaji wa kimkakati katika miundombinu unaweza kubadilisha sura ya taifa.

Jua linapoanza kuchomoza juu ya Bahari ya Hindi na mwanga wake kugonga nyaya za Daraja la Tanzanite, mamia ya watu huendelea kutembea juu yake.

Wengine wakitafuta afya. Wengine wakitafuta kipato. Wengine wakielekea kwenye shughuli zao za kila siku. Bila kujua, kila mmoja wao anakuwa sehemu ya simulizi kubwa zaidi.

Simulizi ya jinsi daraja moja lilivyoondoa foleni, likafungua fursa za biashara, likahamasisha afya bora na kuwa ishara ya mabadiliko ya Tanzania.

Hiyo ndiyo hadithi ya Daraja la Tanzanite. Hadithi ya miundombinu inayounganisha si tu pande mbili za jiji, bali pia maendeleo na maisha ya wananchi wake. Hakika maendeleo kwenye miundombinu unaweza usiamini ni Tanzania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *