
Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan Ishaq Dar amesema mpango wa amani wa vipengele 20 uliopendekezwa na Rais wa Marekani Donald Trump kwa ajili ya Ghaza sio ule ulioidhinishwa na viongozi wa nchi za Kiarabu na Kiislamu, ikiwemo Pakistan.
“Hii siyo hati yetu,” Dar amewaeleza wanahabari katika mkutano aliofanya nao katika mji mkuu wa nchi hiyo Islamabad.
Amesema, Pakistan na washirika wake wamedai kurejeshwa nukta kadhaa muhimu ambazo hazimo ndani ya hati hiyo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan amesema: “kuna baadhi ya maeneo muhimu ambayo tunataka yashughulikiwe … Kama hayamo, basi yaingizwe”.
Dar amebainisha kuwa, vipaumbele vya haraka vinabaki kuwa ni usitishaji vita, kukomeshwa mauaji ya kimbari, kuruhusu misaada ya kibinadamu iingizwe Ghaza, na kuhitimishwa mpango wa kuwalazimishwa Wapalestina wahame.
Waziri huyo wa mambo ya nje wa Pakistan amelielezea tangazo lililotolewa na Trump akiwa pamoja na Netanyahu kuwa “tangazo kutoka kwa upande wao (wawili hao).” Amesisitiza kuwa Pakistan inatetea taarifa ya pamoja iliyotiwa saini na mataifa mengine saba yenye Waislamu wengi.
“Sisi tunamiliki hii. Ikiwa kuna tofauti yoyote popote pale, tungeipitia – tumejifunga na hii,” ameongezea kusema Dar.
Viongozi wa Uturuki, Pakistan, Saudi Arabia, Qatar, Imarati, Misri, Jordan na Indonesia walikutana na Trump pembeni ya kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, ambapo Trump aliwasilisha mbele ya viongozi hao mpango wake wa vipengele 20 kwa ajili ya Ghaza.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan ameiambia pia tovuti ya habari ya Geo News ya Pakistan kwamba rasimu ya White House “haijumuishi mapendekezo yetu yote.”
Mbali na Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan, Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri Badr Abdelatty naye amesisitiza kuwa mpango wa Trump wa usitishaji vita huko Ghaza una “matundu mengi” ambayo yanahitaji kuzibwa.
Mapema kabla ya hapo, Waziri Mkuu wa Qatar Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al Thani naye pia alieleza wasiwasi aliona juu ya suala hilo. Katika mahojiano na televisheni ya nchi hiyo ya Aljazeera, Abdulrahman Al Thani alisema mpango wa Trump “unafanikisha lengo kuu kwa kuhitimisha vita, lakini kuna baadhi ya masuala ambayo yanahitaji ufafanuzi na mazungumzo”…/