Chanzo cha picha, REUTERS/Stringer TPX IMAGES OF THE DAY
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 3
Baada ya tangazo kuwa Marekani na Iran wameafikia makubaliano, hii ilionekana kama zawadi nzuri kwa siku ya kuzaliwa ya Donald Trump, ambaya anasema pia ushasainiwa.
Kupitia mitandao ya kijamii alipotangaza makubaliano hayo, rais huyo wa Marekani alisema kuwa Mlango bahari wa Hormuz utafunguliwa kwa meli za kibiashara na Marekani itaondoa kizuizi cha kijeshi ambacho kilikuwa kimewekwa eneo hilo dhidi ya bandari za Iran.
Trump aliandika kuwa “wacha mafuta yatitiririke sasa.”
Kulingana na Trump, makubaliano hayo ni mazuri na yataleta amani ukanda huo wote wa Ghuba ya Uajemi.
Ila semi kama hizi si za kushangaza kutoka kwa Trump. Alitoa tangazo sawia kuhusu usitishaji wa vita eneo la Gaza.
Trump alisema kuwa “amani hii itadumu milele, na ni mwanzo wa mwamko mpya” ila uhalisia wa hali eneo la Gaza ni tofauti kabisa na majivuno ya Trump.
Katika mahojiano na shirika la habari la Fox News, naibu rais wa Marekani JD Vance alisema kuwa, “Iran kutomiliki silaha za nyuklia” ni miongoni mwa mapendekezo yaliyokubaliwa.
Suala la kumiliki nyuklia itajadiliwa ndani ya siku 60 zijazo katika muda uliongezwa wa usitishaji mapigano.
Ila baada ya miaka mingi ya kuishinikiza Iran kuachana na mpango wake wa nyuklia, haijabainika wazi kama kiukweli watasitisha mpango huo baada ya makubaliano haya.
Kwa hivyo iwapo Iran itakubali matakwa ya makubaliano hayo, ndiyo itaamua iwapo mkataba huo utadumu au la.
Wataalam wa sekta ya nishati wameonya kuwa, safari za meli kupitia mlango bahari wa Hormuz, huenda zisirejee katika hali ya awali, kwani itachukua muda kupunguza msongamano uliopo na kuzalisha mafuta ya kutosha ili kusambaza kama ilivyo kuwa awali kabla ya vita kuanza.
Ikiwa imesalia siku chache kabla ya mkataba wa Iran na Marekani kutiwa Saini, Mataifa hayo mawili bado yako na muda wa kuainisha masuala tata, na muda huu pia ni tete kwani makubaliano hayo yanaweza kusambaratika.
Ila kizuizi kingine katika vita hivi ni Israel.
Vita hivi vimekuwa vya pande tatu. Gazeti la Wall Street Journal lilichapisha siku ya Jumapili kuwa Rais Trump alikuwa amejawa na ghadhabu baada ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kuamrisha mashambulizi nchini Lebanon, na kusema ilikuwa inahatarisha makubaliano yaliyoafikiwa na Iran.
Chanzo cha picha, EPA
Kilichomo ndani ya makubaliano hayo bado hakijawekwa wazi rasmi.
Ila iwapo Israel itaendeleza mashambulizi yake nchini Lebanon, Iran inaweza kuamua kufunga mlango bahari wa Hormuz tena na kuhatarisha uchumi wa dunia.
JD Vance pia katika mahojiano yake alisema, vita hivyo vimewaathiri raia wa Marekani kwa ongezeko la bei ya mafuta.
“Kwangu ni kuwashukuru raia wa Marekani, na sasa bei ya mafuta itashuka tena” alisema Vance.
Kushuka kwa bei ya mafuta nchini Marekani kutasaidia kupunguza shinikizo la kisiasa kwa chama cha Republican wakati wanakaribia uchaguzi wa nusu muhula mwezi Novemba.
Kulingana na kura za maoni, ushawishi wa Trump umepungua. Kura ya maoni iliyofanywa na YouGov inaonyesha kuwa 63% ya raia wa Marekani hawajafurahishwa na jinsi Trump anaendesha uchumi wa taifa hilo, huku 57% wakiamini uchumi wa taifa hilo unadorora.
Ila makubaliano ya Iran na Marekani yanatarajiwa kubadilisha hali, na kupunguza shinikizo la kiuchumi na kisiasa iwapo bei ya mafuta itashuka, na kumpa Trump afueni ya kisiasa.