Afrika Kusini. Wakati muziki wa Afrika Kusini ukiendelea kutamba katika mataifa mbalimbali Afrika. Baadhi ya wasanii wa nchi hiyo wanaanza kukumbana na changamoto mpya baada ya matamasha yao kufutwa kutokana na mtazamo unaoendelea kujengeka kuwa taifa hilo lina chuki dhidi ya wageni.

Hali hiyo imeilazimu Serikali ya Afrika Kusini kuvunja ukimya na kueleza wasiwasi wake, ikisema taswira hiyo imeanza kuathiri moja kwa moja sekta ya sanaa na burudani pamoja na fursa za wasanii wake katika soko la Afrika.

Waziri wa Sheria na Maendeleo ya Katiba, Mmamoloko Kubayi amesema baadhi ya wasanii wamemfikia binafsi, wakilalamikia kupoteza maonyesho katika nchi mbalimbali za Afrika baada ya waandaaji wa matamasha kufuta mipango yao ya awali.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, kufutwa kwa maonyesho hayo kumewaathiri wasanii kifedha na kupunguza nafasi zao za kuendelea kukuza ushawishi wa muziki wa Afrika Kusini nje ya mipaka ya nchi hiyo.

Kubayi amesema ni jambo la kusikitisha kuona matukio yanayohusishwa na chuki dhidi ya wageni, sasa yanaanza kuathiri hata sekta ya sanaa.  Ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikitumika kuunganisha watu wa mataifa tofauti kupitia sanaa na utamaduni.

Amesisitiza kuwa Afrika Kusini si taifa lenye chuki dhidi ya wageni kama inavyodaiwa na baadhi ya watu. Akionya kuwa kuendelea kwa mtazamo huo kunaweza kuharibu uhusiano wa nchi hiyo na mataifa mengine ya Afrika.

Mbali na burudani, amesema taswira hiyo inaweza pia kuathiri biashara, utalii na uwekezaji. Huku akiitaka jamii kushughulikia masuala ya uhamiaji kwa kufuata sheria badala ya kutumia kauli au vitendo vinavyoweza kutafsiriwa kama ubaguzi.

Kauli hiyo imekuja wakati kukiwa na mjadala mpana kuhusu nafasi ya Afrika Kusini ndani ya bara la Afrika. Huku wadau wa burudani wakisisitiza kuwa muziki na sanaa vinapaswa kubaki kuwa daraja la kuunganisha watu na siyo chanzo cha mgawanyiko

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *