Mamlaka husika katika Jimbo la Borno kaskazini mashariki mwa Nigeria zimearifu kuwa karibu wapiganaji 10,000 wa zamani wa kundi la waamgambo wa Boko Haram sasa wameunganishwa tena katika jamii chini ya mpango unaofadhiliwa na serikali wa kurekebisha tabia na kuhimiza kuachana na makundi ya uasi.

Tangazo hilo limetolewa kufuatia wanamgambo 720 wa zamani wa kundi la Boko Haram kuhitimu mafunzo katika kituo cha kurekebisha tabia huko Maiduguri, makao makuu ya jimbo la Borno kaskazini mashariki mwa Nigeria, katika hafla iliyohudhuriwa na maafisa wa serikali.

Mamlaka husika katika jimbo la Borno zimeeleza kuwa, kundi hilo la hivi karibuni la wanamgambo wa Boko Haramu waliopata mafunzo ya kurekebisha tabia na kuuungana tena na jamii katika maisha ya kiraia linaifanya jumla ya idadi ya waasi wa zamani wa kundi hilo la kitakfiri waliojumuishwa tena katika jamii zao kufikia 9,680.

Mpango huu ni sehemu ya juhudi kubwa za Nigeria za kudhoofisha akundi ya wanamgambo wenye silaha wanaofanya hujuma katika eneo la Ziwa Chad. Mpango huu umekuwa ukiwahimiza wanamgambo wenye silaha kujisalimisha na kurejea katika maisha ya kiraia.

Picha zilizorushwa kutoka kwenye hafla hiyo zimeonyesha mamia ya wanamgambo wa zamani wa Boko Haram wakiwa wamekusanyika katika kituo cha mafunzo ambapo washiriki walikula kiapo kabla ya kuachiliwa rasmi kwa jialiya kujiunga na jamii.

Hujuma za Boko Haram, zilizoanza zaidi ya muongo mmoja uliopita kaskazini mashariki mwa Nigeria, zimeua makumi ya maelfu ya watu na kupelekea mamilioni ya wengine kuyahama makazi yao nchini humo na kukimbilia katika jirani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *