
Siku mia moja na sita baada ya kuanza hujuma za kijeshi za Marekani na Wazayuni dhidi ya Iran, hatimaye Tehran na Washington zimefikia muafaka katika mfumo wa makubaliano ya kuhitimisha rasmi vita hivyo.
Zaidi ya yote, yaliyomo katika makubaliano hayo na matokeo yake yanatoa changamoto kwa simulizi kuu ya “washindi” na “walishindwa” katika mgogoro huu ambao haujawahi kutokea huko nyuma. Vita vilivyoanza asubuhi ya tarehe 28 Februari 2026, kwa msingi wa malengo yaliyotangazwa rasmi na ya siri ya Marekani na utawala wa Kizayuni, halikuwa jambo dogo bali ni mradi mkubwa uliokusudiwa kubadilisha mfumo unaotawala nchini Iran. Mashambulizi makali ya kushtukiza na ya moja kwa moja kwenye makazi ya Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi yaliyopelekea kuuawa kwake shahidi, mauaji ya makamanda wakuu wa kijeshi, kulengwa vyombo vya sheria, usalama na vituo vya kijeshi, uharibifu wa miundombinu ya viwanda na huduma za mijini, pamoja na jaribio la kuibua mshtuko wa kisaikolojia katika jamii ya Iran, yote hayo yanaweza kuchambuliwa ndani ya mfumo wa mkakati ambao unatajwa katika fasihi ya usalama ya Marekani kama “pigo la kupoozesha.” Mkakati ambao lengo lake kuu lilikuwa ni kuupindua utawala wa Jamhuri ya Kiislamu au kwa uchache kuilazimisha Tehran isalimu amri na kukubali masharti ya Washington. Lakini kile kilichotokea baadaye kilikuwa tofauti kabisa na mahesabu ya awali ya wapangaji vita.
Majibu ya Iran hayakuwa ya kujitetea tu. Kwa kulenga vituo 18 vya Marekani katika nchi nane za eneo, Tehran ilipanua wigo wa vita nje ya mipaka yake ya kitaifa na hivyo kuitwisha Washington gharama za moja kwa moja za uwepo wake wa kijeshi Asia Magharibi. Muhimu zaidi ni kwamba udhibiti na kufungwa Lango-Bahari la Hormuz, njia kuu ya usafiri wa nishati, kuliyatumbukiza masoko ya kimataifa katika hali ya wasiwasi na ukosefu wa utulivu, hali ambayo tayari wachambuzi wengi wa nchi za Magharibi walikuwa tayari wameonya kuhusiana nayo. Miaka kadhaa iliyopita, taasisi za utafiti kama vile RAND, Brookings, na Kituo cha Mafunzo ya Kimkakati na Kimataifa zilisisitiza katika ripoti yazo kwamba vita vyovyote vikubwa dhidi ya Iran vinaweza kusababisha usumbufu katika usafirishaji wa nishati, kupanda kwa bei ya mafuta, matatizo katika mzunguko wa usambazaji bidhaa kimataifa, na kuibua mzozo wa kikanda. Sasa maonyo hayo yamethibitika kuwa ya kweli.
Kwa mtazamo huu, matokeo muhimu zaidi ya vita vya hivi karibuni yanapaswa kutathminiwa kama ufichuzi wa makosa mawili makubwa yaliyofanywa na Marekani kuhusu Iran. La kwanza ni dhana kwamba jibu la Tehran kwa uchokozi wa maadui lingekuwa dogo na dhaifu. Kosa la pili ni kudhani kwamba muundo wa kisiasa na kiusalama wa Iran ungesambaratika kutokana na mashinikizo ya mapigo mazito ya awali au ungesalimu amri ili kuepusha gharama zaidi. Lakini sio tu hilo halikutokea, bali Jamhuri ya Kiislamu iliweza kudumisha mshikamano na umoja wake wa kitaifa na kukarabati haraka muundo wake wa kamandi, huku ikisimamia vilivyo masuala ya nyanjani na diplomasia.
Makubaliano ya kumaliza vita yamefikiwa katika hali ambayo malengo ya awali ya Marekani yalikuwa hayajafikiwa. Utawala uliopo haujabadilika, makombora na silaha nyingine muhimu za Iran zingalipo, ushawishi wake kieneo haujaharibiwa, na Jamhuri ya Kiislamu haikukubali masharti ambayo Washington ilikuwa imeiwekea mwanzoni mwa vita. Kinyume chake, Marekani imelazimika kukubali na kutia saini mapatano ambayo yanatambua uwepo na kudumu kwa Jamhuri ya Kiislamu kama ukweli usiopingika.
Radiamali ya jamii ya kimataifa pia ni muhimu. Takriban wahusika wakuu wote wa kimataifa, kuanzia nchi za kikanda hadi mataifa yenye nguvu ya Asia na serikali za Ulaya, wamekaribisha mapatano haya ya kumaliza vita, ukiachilia mbali utawala haramu wa Israel; mchochezi mkuu wa vita ambaye tangu mwanzo wa mgogoro alikuwa amewekeza pakubwa kisiasa na kiusalama katika kuendeleza makabiliano na kuzidisha mashinikizo dhidi ya Iran. Makaribisho haya ya kumalizika vita yamebeba ujumbe wa wazi. Bila kujali tofauti za kisiasa na Tehran, walimwengu wanaona kuwa uthabiti katika eneo hili ambalo ni moja ya kanda za kistratijia zaidi duniani, hauwezekani bila ya ushirikiano na nafasi ya Iran.
Kwa maneno mengine ni kuwa, vita vilivyolazimishwha na Marekani na Israel dhidi ya Iran si tu kwamba havikuiondoa Iran katika mlingano wa kieneo, bali pia vimeonyesha kwa mara nyingine tena kwamba hakuna utaratibu wa usalama endelevu katika eneo la Asia Magharibi unaoweza kufikirika bila ya kuzingatia uzito wa kijiografia wa Jamhuri ya Kiislamu. Ushindi katika vita haupimwi tu kwa idadi ya majeruhi au kiwango cha uharibifu wa miundombinu. Katika fasihi ya taaluma ya kimkakati, mshindi wa kweli ni upande unaoweza kufikia malengo yake ya kisiasa na kuzuia upande mwingine kufikia malengo yake. Iwapo tutakichukulia kigezo hiki kama msingi, swali muhimu hapa ni je, ni kwa kiwango gani Marekani na utawala wa Kizayuni ziliweza kufikia malengo yao yaliyotangazwa hadharani na yaliyofichika? Je, ziliweza kuupindua mfumo wa kisiasa wa Iran? Je, zilifanikiwa kuilazimisha Tehran isalimu amri? Je, ziliweza kuvuruga ushawishi wa kieneo na uzuiaji humuma wa Jamhuri ya Kiislamu? Jibu la maswali haya yote ni hasi, kwa uchache kwa kutilia maanani ukweli uliopo. Hii leo baada ya kupitia moja ya vipindi vigumu zaidi katika historia yake ya sasa, Iran haiko tena katika nafasi ya nchi iliyosalimu amri, bali iko katika nafasi ya mhusika mkuu ambaye kwa kulinda muundo wake wa kisiasa na uwezo wake wa kistratijia, ameweza kuilazimisha Marekani kuhitimisha vita kwa masharti ya Iran. Kukubalika kusiko na kifani kimataifa kwa mapatano ya kuhitimisha vita, sio kukaribisha tu mwisho wa mzozo uliopo, bali pia ni kukiri kwa njia isiyo ya moja kwa moja ukweli kwamba, licha ya mashinikizo na gharama zote, lakini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inasalia kuwa miongoni mwa wachezaji wakuu wa kijiopolitiki katika mojawapo ya maeneo nyeti zaidi duniani. Historia imesajili mapatano haya kama hati ya kushindwa mahesabu ya nguvu ambayo ilidhani kwamba ingeweza kuifuta Iran katika milinganyo ya kieneo; lakini hatimaye ikalazimika kukiri ukweli wa uwepo wake kupitia makubaliano rasmi.