
Viongozi wa Afrika siku ya Jumanne walikutana katika mkutano wa dharura wa ngazi ya juu uliofanyika kwa njia ya mtandao, kwa lengo la kutafuta ufadhili wa dola milioni 518 za kudhibiti mlipuko wa Ebola unaoendelea huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Uganda.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi, mlipuko huo umefikia visa 827 na kusababisha vifo karibu 200. Mkutano huo uliofanyika kwa njia ya intaneti umesisitiza umuhimu wa kuimarisha mipango ya kitaifa na kikanda ya kukabiliana na janga hilo, kuimarisha uratibu wa mipakani, pamoja na kuongeza maandalizi, ufuatiliaji na hatua za kuzuia maambukizi.
Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, amesema: “Kuchelewa katika kuchukua hatua kunaweza kugeuza mlipuko wa eneo moja kuwa mgogoro wa kikanda na hata wa kimataifa. Ndiyo maana juhudi zetu zinapaswa kulenga kuvunja mnyororo wa maambukizi na kuuzuia Ebola katika chanzo chake.”
Katika kikao hicho, Ramaphosa alitangaza kuwa nchi yake itaongeza mchango wake kutoka dola milioni 5 hadi dola milioni 13.5.
Jean Kaseya, Mkurugenzi Mkuu wa Vituo vya Afrika vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC), amesema mlipuko huo lazima udhibitiwe haraka iwezekanavyo ili kuepusha hali mbaya zaidi kama ilivyoshuhudiwa Afrika Magharibi na mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika milipuko ya awali ya bara hilo.
Mkutano huo uliitishwa na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) ambaye pia ni Rais wa Burundi, Evariste Ndayishimiye. Pia ulihudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Felix Antoine Tshisekedi Tshilombo, pamoja na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, viongozi wa nchi mbili zinazokumbwa kwa sasa na mlipuko huo.
Mkutano huo ulitumika kama jukwaa la kuimarisha dhamira ya kisiasa, kuhamasisha rasilimali za kifedha, na kuratibu msaada wa kiutendaji, kwa lengo la kuimarisha mwitikio wa pamoja wa Afrika dhidi ya mlipuko huo na kuimarisha usalama wa afya wa bara zima.