Serikali ya Somalia imetoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuheshimu sheria za kimataifa, kutambua mamlaka yake ya kitaifa, na kulaani hatua zozote zinazodhoofisha umoja na uthabiti wa taifa hilo.

Katika taarifa iliyotolewa mjini Mogadishu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya Somalia ilieleza wasiwasi kuhusu mawasiliano ya hivi karibuni ya kidiplomasia kati ya utawala wa Israel na eneo la Somalia lililojitenga na kujitangazia uhuru la Somaliland. Taarifa hiyo imesema kuwa hatua hizo zimefanyika nje ya mfumo unaotambuliwa na serikali ya shirikisho ya Somalia.

Mvutano kati ya Somalia na utawala haramu wa Israel uliongezeka baada ya eneo hilo la Somaliland kufungua rasmi ubalozi mpya mjini Al Quds (Jerusalem) siku ya Jumatatu, kufuatia uamuzi wa Israel kuitambua Somaliland kama dola huru.

Taarifa hiyo imesema “Somalia ni taifa huru linalotambuliwa kimataifa, na serikali yake ndiyo mamlaka pekee halali yenye uwezo wa kuiwakilisha nchi katika mahusiano ya kimataifa.”

Wizara hiyo ilisisitiza kuwa mahusiano yoyote ya kisiasa au kidiplomasia na eneo hilo lililojitenga bila idhini ya Mogadishu ni kinyume na sheria za kimataifa na hayana uhalali wa kisiasa.

Israel ilitangaza kuitambua Somaliland kama dola huru mnamo Desemba 2025, hatua ambayo Somalia iliipinga na kuilaani vikali, ikiitaja kuwa ni “shambulio la makusudi dhidi ya mamlaka na uhuru wa Somalia.” Aidha nchi za Afrika, Kiarabu na Kiislamu duniani zimepinga vikali hatua ya utawala wa Israle kuanzisha uhusiano na eneo la Somaliland ambalo ni sehemu ya Somalia.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *