Njombe. Watu wawili wanaokadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 35 na 36 wamekutwa wameuawa katika eneo la Msete, Kata ya Mji Mwema, mkoani Njombe, huku pembeni mwa miili hiyo kukiwa na viroba vinne vya parachichi.

Tukio hilo limetokea siku chache baada ya wakazi wa Mkoa wa Njombe, ambao wengi wao ni wakulima wa parachichi, kulalamikia ongezeko la wizi wa matunda hayo mashambani, hali inayowalazimu baadhi yao kulala mashambani kuyalinda.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 17, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Mahamoud Banga, amesema Jeshi la Polisi linaendelea kuwatafuta watu wanaohusika na mauaji hayo ili wachukuliwe hatua za kisheria.

Baadhi ya viroba vilivyokuwa na parachichi ndani vikiwa eneo ambalo miili ya marehemu hao ilikutwa huko Msete Mji Mwema halmashauri ya mji wa Njombe.

Banga amesema kuwa Juni 15, 2026, majira ya mchana, Jeshi la Polisi lilipokea taarifa kuhusu kuwepo kwa miili miwili ya wanaume katika eneo la Msete, Mtaa wa Mji Mwema, Halmashauri ya Mji wa Njombe.

Amesema baada ya kufika eneo la tukio, askari walikuta miili hiyo ikiwa na majeraha kichwani na sehemu mbalimbali za mwili.

Banga amesema miili hiyo ilikuwa imetelekezwa eneo hilo huku karibu vinne hivyo.

“Jeshi la Polisi Mkoa wa Njombe linaendelea na uchunguzi wa tukio hili ili kubaini wahusika na kuhakikisha hatua stahiki zinachukuliwa kwa mujibu wa sheria,” alisema Banga.

Aidha, Kamanda Banga amewaomba wananchi kufika Hospitali ya Kibena iliyopo Halmashauri ya Mji wa Njombe kwa ajili ya kutambua miili hiyo, ambayo hadi sasa haijatambulika.

Baadhi ya viroba vilivyokuwa na parachichi ndani vikiwa eneo ambalo miili ya marehemu hao ilikutwa huko Msete Mji Mwema halmashauri ya mji wa Njombe.

Pia, ametoa wito kwa wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi, akisisitiza kuwa Jeshi la Polisi halitasita kuwachukulia hatua za kisheria wale wote watakaobainika kufanya vitendo hivyo.

James Mhenga, mkazi wa eneo hilo amesema walikuta miili ya watu hao katika eneo hilo na kubaini kuwa marehemu hao si wakazi wa eneo hilo.

“Tumeikuta miili hiyo hapa, lakini si wakazi wa eneo hili. Huenda waliuawa kwa kudhaniwa ni wezi wa parachichi,” alisema Mhenga.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *